Uongozi wa klabu ya Simba umefikia makubaliano ya kuvunja mkataba na mshambuliaji Pa Omar Jobe (25) baada ya kipindi kifupi cha miezi sita. Jobe alijiunga na Simba akitoke katika timu ya Zhenis inayoshiriki Ligi Kuu nchini Kazakhstan.
Baada ya kutua Unyamani ambapo alianza kwa kuonesha kiwango kizuri lakini baadae mambo yakaanza kuharibika. Akiwa Simba Jobe alipoteza hali ya kujiamini, alipoteza nafasi na ufanisi wake ulikuwa unapungua siku hadi siku.
Kutokana na kuporomoko kwa kiwango chake, mashabiki wa Simba walianza kumponda nje ya uwanja na kupoteza matumaini nae, huku wengine wakianza kushinikiza uongozi wao umwache mchezaji huyo.
Moja ya Mashabiki ambao walikuwa mstari wa mbele kumpa makavu Jobe ni Kay Mziwanda ambaye popote alipokuwa alijivisha mabomu na miwani ya chuma, kisha kuanza kumkataa hadharani ikiwemo kwenye mitandao yake ya kijamii.
Akihojiwana Waandishi wa Habari mwishoni mwa msimu katika dimba la Azam Complex Chamazi, Mziwanda alisema kwamba “Aliyemleta Jobe Simba atafutwe, alitumia vigezo gani kumsajili mchezaji kama huyo”
“Nimetafuta hata video zake Youtube hazipo, hakuna hata moja, yule Jobe sio mchezaji wa kuvaa jezi ya Simba” Alisema Kay Mziwanda Shabiki wa Simba.
Simba wameendelea kutangaza kuachana na wachezaji wake hadi sasa wametangaza kuachana na wachezaji kadhaa akiwemo, Luis Miquissone, Saidoo Ntibazonkiza, John Bocco, Kennedy Juma.