Dar es Salaam. Ndugu wa kada wa Chadema, Kombo Mbwana wamesimulia jinsi ndugu yao alivyokamatwa na watu wasiojulikana Juni 15, 2024 na hatimaye Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga kukiri kumshikilia.
Jumapili iliyopita, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, ACP Zacharia Bernard alitoa taarifa kwa vyombo akieleza kumshikilia Kombo kwa tuhuma za kutumia vifaa vya kielektroniki pamoja na laini za simu za mitandao mbalimbali zisizo na usajili wake katika kutekeleza uhalifu huo, kinyume cha sheria za nchi.
Taarifa hiyo iliibua hisia za utekaji kwa Jeshi la Polisi. Hata hivyo, akizungumza jana Julai 15, 2024 mkoani Simiyu akiwa katika ziara ya kuzungumza na maofisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Camilius Wambura alisema jeshi hilo halihusiki na utekaji, bali limekuwa likiwaokoa wanaotekwa.
Leo, Jumanne Julai 16, 2024, Mwananchi limezungumza na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi aliyesema taarifa walizotoa ni za awali na uchunguzi unaendelea.
“Tumetoa taarifa za awali, uchunguzi ukikamilika tutatoa taarifa kamili,” amesema.
Akizungumza na Mwananchi leo Julai 16, 2024, Hellena Joseph, mama mzazi wa Kombo amesema waliruhusiwa kuonana na mwanaye baada ya kukwama jana.
“Nimeonana na Kombo, amenisimulia mateso aliyopewa. Amesema alikamatwa Juni 15, 2024 Jumamosi. Walisema hilo eneo ni la kwao na lina ukubwa wa ekari tatu, lakini aliyewauzia wamemsahau. Kombo aliwaambia si kweli, hili eneo ni la familia.
“Ndipo wakamchukua wakaenda naye barabarani ili wamwonyeshe nyaraka, wakaanza kuzozana, yule dereva aliyekuwa akiendesha lile gari ni mtu aliyeshiba, akafungua mlango na kumsukumiza ndani ya gari na kuanza kumpiga huku wakiondoka,” amesimulia.
Amesema mwanaye amewaambia kuwa akiwa kwenye gari walimchukulia simu na pesa zake, ingawa hakuwaambia ni shilingi ngapi.
“Amesema pia alikuwa na koti lake nalo wamechukua. Ametusimulia wamemzungusha mikoa 10, kila mkoa wanaofika wanampiga wanamuuliza, wewe ndiye Kigogo? “Walikuwa wakimlazimisha kuweka saini kwenye makaratasi yao, akikataa wanampiga mpaka kidole cha mkono wa kulia kimelemaa,” amesema.
Kuhusu kula, amesema mwanaye aliwaeleza alikuwa akila kwa taabu, “mwenyewe anasema chakula pia walikuwa hawampi anachotaka, hata jana baada ya sisi kufika pale kituoni alikuwa anasikia njaa sana.
“Anasema kuna chakula alikuwa akiletewa, lakini anakikataa anasema hakiwezi, analazimishwa kula hivyo hivyo. Aliwaomba hela zake, ili anunue chakula, walikataa,” amesema mama huyo na kuongeza;
“Kwa kweli afya ya Kombo imedhoofika sana. Mimi mwenyewe mama yake nimehuzunika sana baada ya kutoka pale kituoni nimeshikwa na majonzi sana.
“Pia kidole gumba cha mkono wa kulia kimelemaa. Tulipomuuliza, alisema mwili wote unauma, walikuwa wanamfunga miguu ananing’nia huku anachapwa fimbo,” amesimulia.
Maelezo ya mama huyo yanafanana na ya Katibu wa Chadema Mkoa wa Tanga, Michael Haule aliyesema kuwa Kombo amewasimulia kuwa alifungwa kitambaa cheupe muda wote aliokuwa akisafirishwa kwenye mikoa 10 aliyodai kufikishwa.
“Walipomchukua wakamfunga kitambaa cheusi na hakujua anakwenda wapi, anasema hicho kitambaa wamemvua juzi baada ya kaimu RPC kutangaza kuwa wamemkamata.
“Ametueleza wamemtishia kwamba asije kuongea na waandishi wa habari watakapomtoa mahabusu, vinginevyo watamuua,” amedai.
Amesema wamemwombea dhamana, lakini wamekataliwa. “Wamesema jalada lake lipo kwenye uchunguzi na wakikamilisha watampeleka mahakamani. Hapa tupo kwenye mchakato wa kufungua kesi.”
Kwa upande wake, Wakili Michael Lugina anayefuatilia suala hilo, amesema wanafanya mchakato wa maombi ya kuwataka polisi wampeleke mahakamani.
“Tunataka kufungua kesi kwa sababu tayari ameshikiliwa na amekaa mahabusu kinyume na sheria. Leo inaweza ikashindikana, lakini mpaka kesho asubuhi itawezekana. Ikiwa kesho (leo) watampeleka mahakamani atapata uwakilishi wa kisheria, lengo ni kumfikisha mahakamani na apate haki zake.
“Tumechelewa mahakamani kutokana na kutafuta taarifa, kwa sababu ili upeleke maombi ni lazima uwe na taarifa kamili zisiwe za kubahatisha kwa sababu polisi nao wana haki zao,” amesema.
Akizungumza na Mwananchi Juni 15, 2024, mke wa Kombo, Mariam Rajabu (20), alisema siku hiyo alipokuwa akifanya usafi nyumbani kwao alifika mtu aliyehoji nani anayejenga msingi wa nyumba, alimjibu ni mama na mume wake.
Alidai maswali yalipokuwa mengi, alimuita mume wake aliyekwenda kumsikiliza.
Kwa mujibu wa Mariam, mtu huyo alimweleza mumewe kuwa eneo hilo ameuziwa pamoja na shamba na kama atahitaji kuona nyaraka, waende kwenye gari lililokuwa limeegeshwa jirani na nyumba yao akazione.
“Basi wakaondoka kuelekea kwenye gari huku wakionyeshana eneo na alipoingia tu kwenye gari, nilishtuka kuona gari hilo linaondoka kwa kasi,” alidai na tangu wakati huo hakumuona tena.