Tanzania, Oman zafungua anga, zaondoa ukomo idadi ya safari za ndege

Dar es Salaam. Tanzania na Oman zimesaini mkataba wa usafiri wa anga (Basa) ambao utawezesha mashirika ya ndege kutoka nchi hizo, kusafiri pande zote bila kujali idadi ya safari wala ukubwa wa ndege husika.

Kusainiwa mkataba huu pia kutawezesha mashirika ya ndege yasiyokuwa na ndege kuungana na yale yanayozimiliki kuendesha biashara kwa pamoja.

Mkataba huo umesainiwa jana jijini hapa mbele ya Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Godius Kahyarara.

Akizungumza katika hafla hiyo, Profesa Mbarawa amesema mkataba huo ni maboresho ya uliokuwapo awali uliosainiwa mwaka 1982 ambao umeonekana kupitwa na wakati.

 “Mkataba huu sasa utawawezesha wadau wa anga kuzingatia maeneo mbalimbali ya ushirikiano ikiwemo juhudi za kukuza usafiri na utalii, kushirikiana kuchambua data, matumizi ya miundombinu ya viwanja vya ndege, mafunzo, ubunifu, teknolojia na kuboresha huduma kwa wateja,” amesema Profesa Mbarawa.

Mbali na hilo, mkataba huo unakwenda kuwezesha  biashara kufanyika kwa uhuru bila kuwekwa ukomo wa safari kwa kutumia viwanja sita vya ndege.

Kwa upande wa Tanzania utatumika  Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Abeid Amaan Karume (AAKIA) na wa Kilimanjaro (KIA).

Kwa upande wa Oman viwanja vitakavyotumika ni Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Muscat (MCT), wa Salalah (SLL) na wa Sohar (OHS).

“Vipengele hivi vinafanya mkataba wetu uliosainiwa kuwa rahisi na wenye mwelekeo wa kibiashara ambao unatoa manufaa kwa wadau wa usafiri wa anga kwa kupanua masoko na uendeshaji wa usafiri wa anga,” amesema Profesa Mbarawa.

Amesema anaamini kuongezeka kwa safari za moja kwa moja kati ya nchi hizo kutaongeza idadi ya watalii nchini Tanzania wanaotoka Asia, Ulaya na kwingineko duniani kupitia mitandao ya ndege.

“Wakati tunatekeleza ahadi yetu kwa Air Tanzania Company ya kuanza safari za moja kwa moja hadi Oman katika siku za usoni pia tunaitaka Oman Air kuongeza safari za moja kwa moja kutoka Oman hadi Tanzania,” amesema Profesa Mbarawa.

Rais wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Oman, Naif Bin Hamed Al-Abri amesema makubaliano hayo yanafungua ukurasa mpya katika maendeleo ya huduma za anga na kukuza uchumi wa pande zote mbili.

“Kwa niaba ya Serikali ya Oman natoa wito kwa mashirika yote ya ndege ya pande zote mbili kuboresha shughuli na kuongeza safari zake kati ya nchi hizi mbili ili kukuza shughuli za kijamii, kiuchumi na utalii,” amesema Al-abri.

Awali, akifafanua baadhi ya yaliyoboreshwa katika mkataba huo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Daniel Malanga amesema mbali na kutokuwapo ukomo wa safari za ndege zitakazofanywa kati ya mashirika ya ndege ya nchi hizo, pia mkataba huo umeweka kipengele cha ushirikiano kwa mashirika ya ndege ambacho awali hakikuwepo.

Hiyo inamanisha kampuni mbili hadi tatu zinaweza kutumia ndege moja kufanya biashara kwenda nchi mbalimbali na hiyo si kwa kwenda Oman pekee pia kuna nchi nyingine ya nyongeza.

“Hata kama shirika la ndege kwa sasa halina uwezo wa kutoa huduma za ndege inaweza kuingia mkataba na kampuni yenye ndege kufanya biashara kati ya nchi hizi mbili na moja ya nyongeza,” amesema Malanga.

Amesema maboresho mengine yaliyofanyika ni kuondoa ukomo wa mashirika ya ndege yanayofanya safari zake kati ya Tanzania na Oman hivyo  shirika lolote linaloanzia Tanzania linakuwa mnufaika wa mkataba huo.

Related Posts