TETESI ZA USAJILI BONGO: Yanga kumpeleka Gift APR

BAADA ya beki wa kati Mganda Gift Fred kudaiwa kwamba amekosa namba kwenye kikosi cha Yanga, hivi sasa inaelezwa timu hiyo itamtoa kwa mkopo kwenda kwa mabingwa wa Rwanda, APR.

Beki huyo alijiunga na Yanga wakati wa usajili wa dirisha kubwa, Julai 7, mwaka jana, akitokea SC Villa ya Uganda, lakini inaelezwa atatolewa kwenda Rwanda kutokana na kukosa nafasi kwenye kikosi cha wakali wa Jangwani.

Mkataba wa beki huyo na Yanga unatamatika Juni 2026 na inaelezwa kwamba timu hiyo haina mpango wa kuendelea naye baada ya eneo hilo kutawaliwa na wazawa ambao wanafanya vizuri. Wazawa wanaotesa eneo la ulinzi wa kati ni Ibrahim Abdullah ‘Bacca’, Bakar Mwamnyeto na Dickson Job.

Pamoja na mambo mengine kuondoka kwa Gift kutaipa Yanga nafasi ya kusajili mchezaji mwingine wa kigeni baada ya idadi ya wachezaji 12 kutimia.

Related Posts