WAKURUGENZI TOENI FEDHA ZILIZOTENGWA KWA AJILI YA UTEKELEZAJI WA AFUA ZA LISHE – DKT.DUGANGE – MWANAHARAKATI MZALENDO

 

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Dkt. Festo Dugange amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote Nchini kuhakikisha wanatoa fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa afua za lishe kama zilizopangwa katika bajeti.

 

 

Akifungua Mkutano wa mwaka kwa maafisa lishe wa mikoa na halmashauri nchini leo Julai 16,2024 Jijini Dodoma Dkt. Dugange amewataka wakurugenzi hao kuhakikisha fedha hizo zinatumika kutekeleza shughuli za lishe na kucha tabia ya kuelekeza fedha hizo kufanya mirati mingine.

 

“Baadhi ya wakurugenzi wamekuwa na tabia ya kupeleka fedha za utekelezaji wa afua za lishe kwenye matumizi mengine hivyo ni maelekezo ya Serikali kuhakikisha fedha zote zilizotengwa kwenye bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa afua za lishe zinatumika katika afua hiyo na si vinginevyo” amesisitiza Dkt. Dugange.

 

Amesema Ofisi ya Rais TAMISEMI itafanya tathmini katika Halmashauri zote zilizotenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa afua za lishe, ikibaini fedha hizo kutumika nje ya utekelezaji huo haitasita kuwachukulia hatua wakurugenzi hao.

 

 

Vilevile, amewataka Maafisa lishe nchini kuhakikisha wanaimarisha elimu ya lishe kwa jamii kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu lishe bora kulingana na makundi ya vyakula hasa kwa mama wajawazito, watoto na vijana balee ili kujenga utamaduni wa kutambua umuhimu wa vyakula hivyo.

 

 

Pia, Dkt Dugange amewataka maafisa hao kuhakikisha wanasimamia miradi ya afua za lishe kupitia halmashauri zao ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na Serikali ya kupunguza changamoto ya lishe nchini.

 

 

Aidha, amewataka kuhakikisha takwimu zinazokusanywa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya jamii ni sahihi na zenye ubora ili ziweze kutumika kufanya maamuzi katika ngazi mbalimbali.

 

Related Posts