Wamiliki wa Hoteli Kagera waililia TRA juu ya huduma za EFD

Na Renatha Kipaka, Bukoba

Wamiliki na mameneja wa hoteli mkoani Kagera wameiomba serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuchukua jukumu la kuwa mawakala wa kuuza na kutengeneza mashine za risiti za kielektroniki (EFDs) ili kupunguza usumbufu kwa wafanyabiashara unaotokana na kufuata huduma hizo mbali.

Ombi hilo limetolewa juzi wakati wa kikao baina ya maafisa wa serikali na wadau wa hoteli, ambapo baadhi ya wamiliki na mameneja walisema kuwa kufuata huduma hiyo mbali kumesababisha watumie gharama kubwa.

Afisa Elimu na Mawasiliano kutoka TRA Mkoa wa Kagera, Rwekaza Rwegoshora, amesema serikali imebaini tatizo hilo na kutoa utaratibu kwa mawakala kufungua ofisi kila wilaya na kila mkoa ili kusogeza huduma kwa wananchi.

Kwa upande mwingine, Katibu Tawala Msaidizi anayeratibu masuala ya sekta za viwanda, biashara, uwekezaji, na masoko, David Lyamboko, amewataka watu wenye uwezo wa kuwekeza katika ujenzi wa hoteli kubwa za kitalii kuwasiliana na serikali ya mkoa huu, na kwamba maeneo kwa ajili ya uwekezaji huo yamekwishatengwa.

Jumaa Sadick, mteja wa hoteli na nyumba za kulala wageni, mkazi wa Manispaa ya Bukoba, amesema kuwa pamoja na wawekezaji wa ndani kujituma katika kuwekeza ili kuleta maendeleo, itawabidi wasimamizi wa hoteli wawafundishe wahudumu wao.

“Kuna wakati unakuta mhudumu amefuga kucha na ni mchafu sana, sasa anapoleta chakula na kucha zake hata hamu ya kula inapotea. Usafi wa wahudumu na mazingira ni muhimu,” alisema Sadick.

Sadick ameongeza kuwa kuna kila sababu ya wahudumu hao kutembelewa na afisa afya mara kwa mara ili watu watambue kuwa usafi ni muhimu katika kazi zao.

Related Posts