Said Mwishehe, Arumeru
WANAFUNZI wanaotoka kwenye kaya maskini nchini zaidi ya milioni mbili ni miongoni mwa wafaidikaji wakuu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii(TASAF) imeelezwa.
Aidha wanafunzi hao wanapofika chuo kikuu hupata mkopo kwa asilimia 100 ili kuwawezesha kukamilisha masomo yao kutokana na familia zao kutokuwa na uwezo wa kutoa nyongeza.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa mfuko wa TASAF, Shedrack Mziray, kati ya wafaidikaji wote Milioni5.19 wanafunzi pekee ni Milioni2.13 ambao ni sawa na asilimia 41.
Mziray amesema kati ya wanafunzi 2,139,500 waliohudumiwa, wanafunzi wanawake walikuwa 1,074,445 na wanaume ni 10,65,055 ambao wote wana umri wa kati ya miaka 6 hadi 18.
Amesema mradi huo umetekelezwa katika Halmashauri 186 nchini ambapo pia wanawake ndio wanufaikaji wakuu zaidi ya wanaume.
“Katika idadi hiyo ya wanufaikaji, wanawake ni 2,892,643 sawa na asilimia 55.7 na wanaume ni 2,302,962 ambao ni sawa na asilimia 44.3, hapa utaona Wanawake ni wengi tofauti na wanaume,”amesema.
Aidha Mziray amesema mfuko huo hivi sasa uko kwenye tathmini ya utekelezaji wake ili kuweza kubaini wanufaikaji wanaotakiwa kuondolewa baada ya kufanikiwa kupitia ruzuku ambayo wamekuwa wakipata kupitia TASAF.
” Moja ya sera na masharti ya mfuko wa TASAF ni kuwanyanyua wahitaji kutoka hali duni kwenda katika hali ambayo ataweza kujitegemea kiuchumi, hivyo hivi sasa hadi Septemba 2024 tunatarajia kuondoa wanufaikaji 400,000 ambao hali zao za maisha zimeimarika,” amesema.
Kwa upande wake Sara Mshiu ambaye ni Meneja Akiba na kupunguza umaskini wa kaya wa mfuko wa TASAF anasema moja ya changamoto kubwa walizokabiliana nazo ni uwepo wa kaya hewa ambazo hazistahili kupata msaada kupitia mfuko huo.
Hata hivyo amesema baada ya kubaini hilo, mfuko ulitengeneza mfumo dhabiti wa kubaini kaya hizo na umeweza kuziondoa kwa zaidi ya asilimia 90.
” Changamoto kubwa ilikuwa ni kuingizwa kwa kaya hewa, na wakati mwingine baadhi ya viongozi waliokuwa wakiratibu kuandikisha majina walishindwa kuwaondoa kwa kuogopa hadi uchawi, lakini baada ya kutengenezwa mfumo mzuri, wote waliondolewa,”amesema Sara.
Mfuko wa TASAF ulianzishwa mwaka 2000 nchini ambapo hivi sasa inatekeleza awamu ya tatu ya mradi huo ulioanza mwaka 2020 na kutarajiwa kutamatika Septemba 2025.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Shedrack Mziray akizungumza na Wahariri pamoja na waandishi wa habari kuhusu Miradi inayosimiwa na Mfuko huo ukiwemo wa kuziwezesha kiuchumi kaya masikini . Wahariri na waandishi hao wapo Mkoani Arusha kwa ajili ya kutembelea wanufaika wa Mfuko huo.
Mmoja ya jengo la bweni la Shule ya Sekondari Oldonyowas lililojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) baada ya Wananchi kuomba kujengewa mabweni pamoja na shule hiyo
Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Shedrack Mziray akifafanua jambo kuhusu ujenzi wa shule ya Sekondari ya Oldonyowas ambayo ujenzi wake umetokana na Mfuko huo.
Baadhi ya Wananchi wa Kata ya Oldonyowas wakiwa makini kuzikiliza taarifa inayohusu Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ambavyo katika kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya elimu mkoani Arusha.
Mwenyekiti wa Kata ya Oldonyowas katika Halmashauri ya Arusha Geofrey Ayo akizungumza wakati maofisa wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wao Shedrack Mziray pamoja na waandishi wa habari walipotembelea shule ya Sekondari Oldonyowas iliyojengwa kwa fedha za Mfuko huo.
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Oldonyowas wakiwa makini kufuatilia maelezo ya Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) hayuko pichani baada ya kutembelea shule hiyo iliyojengwa kwa fedha za Mfuko huo.
Matukio mbalimbali katika picha baada ya waandishi, Wahariri na maofisa wa TASAF walipokuwa katika ziara ya kutembelea miradi na wanufaika wa Mfuko huo.