Youssouph Dabo afichua jambo Azam FC

KOCHA Mkuu wa Azam FC, Youssouph Dabo amefunguka sababu za kumtema aliyekuwa nahodha wa timu hiyo, Daniel Amoah kuwa ni kupisha damu changa huku akikiri kuheshimu makubwa aliyoyafanya ndani ya timu hiyo.

Akizungumza na Mwanaspoti, muda mchache kabla ya kuanza safari kuelekea Morocco ambapo wameenda kuweka kambi ya maandalizi ya msimu ujao, Dabo alisema yeye ndiye aliyetoa uamuzi wa kukatwa kwa mchezaji huyo raia wa Ghana aliyedumu kikosini hapo kwa takribani miaka nane.

“Mimi ndiye niliyetoa mapendekezo ya kuachwa kwa mchezaji huyo ambaye ameitumikia timu hii kwa misimu mitano hadi anaagwa, naheshimu mchango wake amecheza vizuri na kuisaidia timu kwa muda aliokuwepo,” alisema Dabo na kuongeza;

“Muda mwingine timu inakuwa na uamuzi wa kuondoa wachezaji na kusajili wengine, hicho ndio kimefanyika, mimi niliomba iwe hivyo, huu ndio mpira.”

Akizungumzia mpango wao nchini Morocco ambapo ndio wameenda kuweka kambi ya wiki mbili, Dabo alisema wakiwa huko watacheza mechi tatu za kirafiki na wakirejea watacheza moja kabla ya mechi ya Ngao ya Jamii Agosti 8.

“Tumecheza mchezo mmoja wa kirafiki Zanzibar, wachezaji bado hawajafunguka, ninahitaji muda zaidi kuwajenga kwa ajili ya kutengeneza timu ya ushindani, nafikiria tukiwa Morocco tucheze mechi tatu za kirafiki,” alisema na kuongeza;

“Lengo la mechi hizo ni kuendelea kuwapa uzoefu wachezaji wageni ili waweze kuingia kwenye mfumo na kutambua Azam FC inacheza mpira wa aina gani kabla ya mechi za mashindano.”

Kocha huyo raia wa Senegal, alimzungumzia mshambuliaji mpya wa timu hiyo, Jhonier Blanco baada ya kufunga dhidi ya Zimamoto timu yake ikiibuka na ushindi wa mabao 4-0.

“Ni mapema sana kumzungumzia lakini naamini mabao mawili aliyofunga yatamuongezea kujiamini japo ana muda mrefu wa kuzoea mazingira na kuzoeana na wenzake, kikubwa ni kwamba namuona akifunga sana akizoea ligi.”

Kuhusu Ligi ya Mabingwa Afrika timu hiyo ikiwa imepangwa na APR ya Rwanda hatua ya awali, Dabo alisema sio mchezo rahisi kwao lakini yeye pamoja na wachezaji wanatakiwa kuwekeza nguvu huko ili kufikia malengo.

“APR sio timu dhaifu, tunatarajia ushindani lakini mipango yetu ni kuhakikisha tunapata matokeo nyumbani na ugenini ili tutinge hatua inayofuata na hatimaye kufikia malengo ya kucheza hatua ya makundi,” alisema Dabo.

Related Posts