ZIFF YATANGAZA FILAMU ZINAZOWANIA TUZO 2024

*Umoja wa Ulaya kuendelea kushirikiana na Tanzania katika shughuli za Sanaa na Jamii

WAANDAAJI WA Tamasha la Kimataifa la Filamu la Nchi za Jahazi Zanzibar maarufu kama ZIFF ( Zanzibar International Film Festival,) wametangaza filamu 70 kati ya 3000 zilizowasilishwa ambazo zitashiriki katika kuwania tuzo za ZIFF kwa msimu wa 27,2024 utakaofanyika Agosti 1 Hadi 4 visiwani Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari leo katika kituo cha utamaduni cha Ujerumani (Goethe Institut,) wakati wa utangazaji wa filamu zilizotinga katika kinyang’anyiro hicho Mkurugenzi wa Tamasha la ZIFF Hatibu Madudu amesema, kwa mwaka huu filamu zaidi ya 3000 zilikusanywa kutoka Nchi zaidi ya 100 na mabara yote ulimwenguni ambazo ni nyingi zaidi kuwahi kuwasilisha ikiwa zimekusanywa kwa mwezi mmoja pekee.

Amesema, Filamu 70 zilizoingia katika kinyang’anyiro cha kuwania tuzo hizo ni pamoja na filamu bora ndefu, filamu bora Makala, tuzo maalum ya Emerson’s ambayo inatolewa kwa filamu bora kwa upande wa Zanzibar, filamu bora fupi, filamu bora ya hali halisi, filamu bora Afrika Mashariki, muigizaji bora Afrika Mashariki wa kike na kiume, Muigizaji bora wa kike na kiume Tanzania, Tuzo maalum ya Mwenyekiti wa Bodi ya ZIFF ambayo hutolewa kwa waandaaji wa filamu wawili, tuzo ya maisha katika Sanaa, na kwa pekee mwaka huu kuna kipengele kipya cha chaguo la watu itakayoleta msisimko katika soko la Tamthiliya.

“Kuna jumla ya filamu ndefu 25, Makala 13, Thamthiliya10, filamu fupi 22…Kuna viwango vikubwa na ubora katika kazi hizi na zoezi la kupiga kura litaanza tarehe 20 mwezi huu hadi tarehe 3 mwezi ujao hivyo waandaaji na waigizaji watengeneze mikakati ya kupigia debe kazi zao ili ziweze kushinda.” Amesema.

Kuhusu uwasilishaji wa Filamu za Tanzania Madudu amesema kuwa; watayarishaji wamejitokeza kwa wingi na kwa miaka mitatu mfululizo Filamu za Tanzania zimekuwa zikishinda tuzo hizo za kimataifa na kuwataka kuwasilisha filamu nyingi zaidi.

Amesema katika tamasha hilo kutakuwa na siku mahususi ya ‘Zanzibar Day’ itakayofanyika Julai 31 mwaka huu ambapo burudani na filamu mbalimbali kutoka Zanzibar ikiwemo House of Wonders zitaoneshwa na hiyo ni pamoja na Workshop 11 zitakazohusisha mafunzo ya filamu, utengenezaji filamu kwa kutumia simu pamoja na namna ya kukuza sekta ya Sanaa kwa ujumla.

Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU,) nchini Tanzania Ms. Christine Grau amesema, Kauli mbiu ya mwaka huu ya Rejuvenation ‘Kuhuisha’ ambayo imewalenga vijana ni moja ya kipaumbele kikubwa cha EU katika kuwawezesha vijana katika nyanja mbalimbali ikiwemo Sanaa na wataendelea kushirikiana katika tamasha hilo.

Ms. Christine ameeleza kuwa EU itaendelea kushirikiana na Tanzania katika shughuli za sanaa na jamii kupitia miradi mbalimbali ambayo tayari inaendelea ikiwemo ya kuwawezesha wanawake.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa ZIFF Joseph Mwale amesema tamasha hilo lina lengo la kuongeza uelewa wa tasnia ya filamu na kukuza Sanaa ya majahazi ya Bahari ya Hindi ikiwemo Asia ya Kusini, Mashariki, Rasi ya Uarabuni, Ghuba ya Uajemi, Iran, Pakistan, India na visiwa vya Bahari ya Hindi.

“Tamasha litakuwa na majukwaa mbalimbali ikiwemo jukwaa la watoto, wanawake wa vijijini, mbio za ngalawa, mpira wa miguu ufukweni kwa wanawake, majadiliano pamoja na uoneshaji wa filamu za kuvutia za Zanzibar. Amesema.

Amesema tamasha hilo linatarajiwa kuwa na watazamaji takribani 2000 kwa kauli mbiu ya Rejuvenation ‘Kuhuisha’ ambapo filamu 3000 zilipokelewa kutoka maeneo mbalimbali duniani zikiwemo ( Tanzania 62, Uganda 123, Kenya 169, Rwanda 12, Burundi 3 na Afrika Kusini 71,) huku filamu nyingine zikitoka katika mataifa zaidi ya 100 ikiwemo Ujerumani, China, India, Somali, Ghana, Denmark, Senegal, Jamhuri ya Korea, Urusi, Ukaraine, Indonesia, Poland na Uingereza.

Amesema kwa mwaka 2024 Tamasha hilo limebebwa na kauli mbiu ya Uhuishaji wa masuala mbalimbali ambayo yalionekana kusuasua na kwa mwaka huu mambo mapya yameongezwa ikiwemo ushiriki wa Mkutano wa Kimataifa wa Vijana wa Vyombo vya Habari (IYMS,) ambao wataleta vijana 100 kutoka maeneo mbalimbali duniani na kufanya filamu fupi kwa lengo kuhamasisha vijana kote ulimwenguni kutumia filamu na vyombo vya habari kuhamasisha, kuelimisha na kuendesha hatua za masuala muhimu ya kimataifa.

Katika Tamasha hilo Thamthiliya zinazowania tuzo ni pamoja na Ripoti, Bunji, Dhohar, Twisted, na Juakali, huku filamu zikiwa ni pamoja na Gwiji wa Taarab, Zanzibar Untold pamoja na Unbankable.

Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU,) nchini Tanzania Ms. Christine Grau akizungumza katika hafla ya utangazaji wa filamu zitakazowania tuzo za ZIFF 2024 na kueleza kuwa EU itaendelea kushirikiana na Tanzania katika shughuli za sanaa na jamii kupitia miradi mbalimbali ambayo tayari inaendelea ikiwemo ya kuwawezesha wanawake. Leo jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa ZIFF Joseph Mwale akizungumza wakati wa hafla hiyo na kueleza kuwa tamasha hilo lina lengo la kuongeza uelewa wa tasnia ya filamu na kukuza Sanaa ya majahazi ya Bahari ya Hindi ikiwemo Asia ya Kusini, Mashariki, Rasi ya Uarabuni, Ghuba ya Uajemi, Iran, Pakistan, India na visiwa vya Bahari ya Hindi. Leo jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Tamasha la ZIFF Hatibu Madudu akizungumza wakati wa hafla hiyo na kueleza, kwa mwaka huu filamu zaidi ya 3000 zilikusanywa kutoka Nchi zaidi ya 100 na mabara yote ulimwenguni ambazo nyingi zaidi kuwahi kuwasilisha ikiwa zimekusanywa kwa mwezi mmoja pekee. Leo jijini Dar es Salaam.

Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU,) nchini Tanzania Ms. Christine Grau (katikati,) akizindua bango maalum la Tamasha la 27 la ZIFF.

Matukio mbalimbali wakati wa hafla hiyo.
 

Related Posts