ACT Wazalendo kusajili wanachama milioni 10 ziara mikoa 22

Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo kimejipanga kufanya mambo matatu katika ziara yake ya mikoa 22 Tanzania Bara ikiwemo kuhamasisha wananchi kushiriki kupiga kura na kuzilinda katika vituo vya kupigia kura katika chaguzi zinazokuja.

Sambamba na hilo, wamejipanga kusikiliza kero za wananchi na dhumuni lingine ni kusajili wanachama milioni 10 katika ziara hiyo inayotarajiwa kuanza Julai 22  mwaka huu ikiongozwa na kiongozi wa Chama hicho Doroth Semu.

Semu ataambatana na viongozi wengine, akiwemo Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Isihaka Mchinjita, Katibu Mkuu  Ado Shaibu na kiongozi wa Chama mstaafu, Zitto Kabwe na kila kiongozi atakuwa anazunguka mikoa yake.

Akizungumzia shabaha ya ziara hiyo, Dar es Salaam leo Julai 17,2024, Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma kutoka chama hicho, Shangwe Ayo amesema wanataka wananchi wajipange kisawasawa kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu ujao.

“Tumejipanga kuingia katika chaguzi hizo na tunaona kuna haja kwenda katika ziara hii kwa sababu tunaona kabisa Serikali iliyopo madarakani haina nia ya kumkomboa Mtanzania,”amesema Ayo

Ayo amesema Watanzania wengi hasa vijana wamekosa imani ya kupiga kura kwa muda mrefu baada ya kubaini mambo wanayotaka hayaonekani kutokana na viongozi waliopewa dhamana kujisahau.

Katika maelezo yake Ayo amesema wametambua changamoto zinazowakumba Watanzania na kupitia ziara hiyo wameamua kurudi kwao kuwaambia na kuwapa mbinu ya kukiondoa chama tawala madarakani.

Kusajili wanachama wapya milioni 10

Amesema katika ziara hiyo wanalenga kusajili wanachama milioni 10 kuelekea  katika uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu ikiwa ni mipango ya kushinda chaguzi hizo.

“Tunaenda kufanya kazi ya usajili kuanzia katika hii ziara  hadi uchaguzi mkuu wa mwaka 2025  kwa kuwa nia yetu ni kushika dola na tunaamini ili tufikie azma hiyo lazima tuwe na wanachama wa kutosha,”amesema.

Ayo amesema hadi sasa chama hicho kina wanachama milioni moja waliosajiliwa kupitia mfumo wa dijitali lakini kuna baadhi bado hawajafikiwa.

Amedai wanataka kusikiliza kero za wananchi na kuona namna ya kuzitatua kwa sababu kwa sasa hawana msaada baada ya kutelekezwa na Serikali iliyojikita kufanya shughuli nyingine bila kuwajali.

“Wameshindwa kuzitatua kwa hiyo tumejipanga kuwasikiliza kupitia ziara hii na kuwataka washirikiane na chama chetu kupigania Tanzania yenye masilahi ya wote,”amedai.

Ayo amesema itaanza Julai 22 mwaka huu, kuwafikia wananchi na majimbo ya uchaguzi 125 Tanzania bara, Kiongozi wa Chama Semu ataenda mikoa  mitano ikiwemo, Dodoma, Manyara, Singida, Arusha pamoja na Kilimanjaro.

“Makamu Mwenyekiti Isihaka atatembelea mikoa wa kichama Selou, Mtwara, Lindi, Pwani na Mkoa wa Tanga, Ado atafanya ziara mikoa ya Mwanza, Simiyu, Mara, Geita na Kagera, wakati Zitto atakuwa mikoa ya Kigoma, Rukwa, Katavi, Tabora, Shinyanga na Mkoa wa kichama Kahama.”

“Dhumuni kubwa la ziara hii ni kuwaandaa wananchi kufanya uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 na tunalenga kusajili wanachama milioni 10 na kusikiliza kero za wananchi baada ya kuona Serikali kushindwa kuzipatia ufumbuzi,” amedai.

Related Posts