Aisha Masaka atua Uingereza, kukipiga Brighton

KLABU ya BK Hacken ya Sweden imemuuza straika Mtanzania, Aisha Masaka kwa klabu ya Brighton inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake nchini Uingereza.

Mapema leo Hacken imetoa taarifa kuwa imemuuza mchezaji huyo kujiunga na Brighton inayoshiriki Ligi ya Kuu ya Wanawake nchini Uingereza ambayo imemaliza nafasi ya tisa kwenye msimu uliopita.

Straika huyo wa timu ya taifa wanawake, Twiga Stars, alijiunga na Hacken msimu 2022 akitokea Yanga Princess.

Kwa upande wa soka la wanawake, Masaka aliweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na kikosi hicho msimu uliopita.

Hacken amedumu kwa misimu miwili akifanikiwa kufunga mabao manne kwenye Ligi ya Sweden.

Mtanzania huyo msimu ujao anakwenda kuichezea ligi hiyo ambayo inashirikisha timu 12 ikiwemo, Manchester United, City, Arsenal na Chelsea.

Nyota ya mshambuliaji huyo ilianza kuonekana akiwa na Alliance Girls ya mkoani Mwanza ambako alicheza kwa misimu mitatu kuanzia 2018-2021.

Msimu uliofuata Yanga ikamsajili akitokea Alliance ambako alifanya vizuri na kuwashawishi mabosi wa Jangwani.

Mshambuliaji huyo, hakukawia. Msimu wa 2021/22 akaibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania hivyo kushinda tuzo ya kiatu cha dhahabu akiweka kambani mabao 35, akifuatiwa Mtanzania mwenzake, Opah Clement aliyefunga mabao 34.

Ndipo msimu uliofuata Yanga ikamuuza kwenda Sweden ambako licha ya kutocheza kikosi cha kwanza aliweka rekodi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Related Posts