CCM, Dk Tulia wanavyojipanga kumdhibiti Sugu Mbeya Mjini

Licha ya kuwa bado kipenga hakijapulizwa, wanaotajwa zaidi kwenye kinyang’anyiro cha ubunge katika jimbo la Mbeya Mjini kwenye uchaguzi wa 2025 ni Dk Tulia Ackson atakayetetea kiti chake na aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia Chadema, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’.

Siasa katika jimbo hilo zimezidi kupamba moto ambapo Sugu anazidi kujiimarisha kurudi tena bungeni, tayari amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa baada ya kumshinda Mchungaji Peter Msigwa.

Dk Tulia, ambaye pia ni Spika wa Bunge na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), anapambana kutetea nafasi yake katika jimbo hilo, itakayompa uhalali wa kuendelea kuongoza pia nafasi nyingine alizonazo.

Vita ya kumlinda Dk Tulia siyo yake peke yake, ni jambo ambalo baadhi ya viongozi wa CCM katika Mkoa wa Mbeya wamelibeba kama suala la chama, kwa sababu anaupa heshima mkoa huo hasa katika uwakilishi wake IPU.

Mwananchi imefanya mahojiano maalumu na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (Nec) Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela ambaye anaeleza sababu za kutaka Dk Tulia aendelee kuwa mbunge katika jimbo la Mbeya Mjini kwa mara nyingine.

Mwaselela anasema sababu za kumuunga mkono Dk Tulia ni kwamba mbali na kuwa mbunge wa Mbeya Mjini, pia, ni kioo cha jamii kwa wanaMbeya na Watanzania kupitia nafasi yake ya Spika wa Bunge na Rais wa IPU.

“Nafasi alizonazo Dk Tulia, ukiachana na ubunge, ni kubwa, tumepata bahati mbunge wetu wa Mbeya mjini ni Rais wa IPU, kwa nini tuipoteze? Kwenye hili ni lazima tuwe wazi, hatujamzuia mtu kugombea naye, lakini tutamlinda Dk Tulia,” anasema.

Anasema hawatasimama na mtu mwingine kwa kigezo cha demokrasia na hawatamzuia mtu kuchukua fomu, wao watasimama na Spika huyo wa Bunge kuanzia kwenye kinyang’anyiro cha kura za maoni 2025 hadi uchaguzi mkuu.

Kiongozi huyo wa CCM, anasema huo ni msimamo wake na siyo wa chama, kwa kuwa chama kina utaratibu wake wa vikao, yeye anazungumza kama M-Nec akisimama kuhakikisha heshima ya Mbeya inalindwa na kuwa hakubaliani na mtu atakayejitokeza kumpinga Dk Tulia ndani ya chama katika jimbo la Mbeya Mjini.

“Hata kama humpendi basi mpe heshima yake kama Rais wa IPU, kama Spika wa Bunge na kama kioo cha jamii, kwa sababu nafasi alizonazo ni heshima kwa mkoa wote na si jimbo la Mbeya Mjini tu.

“Tunafahamu wapo watu wabishi watajitokeza, tutawajadili vizuri, pia tutajiridhisha kama watu hao sio mapandikizi ni nini? Watasema wanafuata demokrasia, ni sawa, lakini kwa nini waturudishe kule Sugu alikuwa anapitia?” anahoji.

Mwaselela anasema kama Sugu atajitosa kugombea jimbo hilo, hamuoni kama atakuwa mshindani wa Dk Tulia.

Anasema uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, Sugu alibebwa na vita kati ya wanaCCM wenyewe ambao waligawanyika kwenye makundi ya urais, wengine walimtaka X na wengine alimtaka Y.

“Wapo wanaCCM wengine walimpigia kura Sugu, hata yeye analifahamu hilo, kwenye uchaguzi wa mwaka 2015, makundi ya urais ndiyo yalimbeba,” anasema.

Mwaselela anasema hamuoni Sugu kama ni mshindani wa Dk Tulia, akiamini mwaka 2010 na 2015 alibebwa na upepo mbaya ulioikumba CCM, ikagawanyika.

“Uchaguzi wa 2015, Sugu alishinda kwa kubebwa na upepo wa makundi ya urais na si kama alijibeba, makundi yaliyokinzana ndani ya CCM, kukawa na vita ya wenyewe kwa wenyewe, makundi yale yakaanza kuweka watu wao.

“Ule ulikuwa ni mtikisiko mkubwa ndani ya chama, ndipo zikaja harakati za Edward Lowassa (wakati akitafuta urais CCM).”

Anasema wakati ule kulikuwa na majina yanatamkwa waziwazi yakionyesha upande, akiwataja waliokuwa watia nia wa nafasi ya urais kipindi ambacho Jakaya Kikwete alikuwa anamaliza muhula wake na kuondoka madarakani.

Anasema mwaka 2010, pia liliibuka kundi la mbunge aliyekuwa akitetea kiti chake, Benson Mpesya dhidi ya kundi jingine.

“Wengi hawaelewi ni nini kilichokuwa kinampa Sugu umaarufu wakati ule, lakini hayo mambo mawili; makundi ya urais 2015 na mtafaruku wa ndani ya CCM mwaka 2010.

“Kuanzia mwaka 2000, jimbo la Mbeya mjini lilipotea, walileta mgombea ambaye hakuwa mzawa, hakuwahi kuwa na bondi na watu wa Mbeya hadi 2005 walipolirudisha baada ya CCM kumsimamisha Mpesya.”

Anasema mwaka 2010, kulikuwa na mvutano wa ndani ya CCM, wengine wakimtaka Mpesya na wengine wakitaka apitishwe mtu mwingine, jambo lililoibua mtafaruku na mpasuko anaodai ndio ulimpa fursa Sugu, ambaye amezaliwa na kukulia Mbeya.

Mwaselela anasema, watu wa Mbeya japo hawana ukabila, wanapenda mbunge wao awe na bondi na mkoa huo, awe mzaliwa, ameishi au wazazi wake wanaishi Mbeya.

“Mwaka 2020 CCM ikamsimamisha Dk Tulia, tumemleta mgombea ‘smart’ kama huyo halafu eti tukubali Sugu atushinde. Haiwezekani. Sisi hatufanyi siasa za kelele, bali za kisayansi na kura zetu tunaelewa zipo wapi.

“Kubwa kuliko yote, tunajua alipotushindia wakati ule na hatuoni njia ambazo atapita tena ili kushinda, kote huko tumerekebisha na tuna mgombea makini, Sugu atapitia wapi? Mbeya mjini si jimbo la kwenda kichwa kichwa,” anasema.

Alipotafutwa kuzungumzia kauli ya Mwaselela na madai ya kubebwa na upepo mbaya ndani ya CCM, Sugu anasema hawezi kumjibu kada huyo wa CCM, lakini anasema alichokisema kwake ni sawa, lakini ni mtu ambaye hawezi kumjibu.

“Kama kasema hivyo, sawa, ni yeye ndiye anaona hivyo, mimi siwezi kujibizana naye, muda utazungumza,” anasema Sugu.

Kuhusu kugombea ubunge kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 katika jimbo la Mbeya Mjini, Sugu anasema wakati ukifika, chama kikimpa ridhaa atafanya hivyo, kwa kuwa anakubalika na wanaMbeya.

“Mbeya nakubalika na sio Mbeya tu, nakubalika Tanzania, wakati ukifika chama kikanipa ridhaa hiyo nitagombea, kwa sasa bado ni mapema,” anasema.

Mbali na joto la uchaguzi jimbo la Mbeya Mjini, Mwaselela anasema kila kitu kinakwenda vizuri, hali ni shwari na tulivu ndani ya chama hicho kwenye majimbo mengine ndani ya Mkoa wa Mbeya kuelekea 2025.

“Hakuna makundi ya urais na mwaka 2025, Rais ni mmoja tu, Samia Suluhu Hassan, pia kiongozi huyu na mwenyekiti wetu wa chama aliusimamia uchaguzi wa ndani kwa weledi mkubwa, kwa kuwa huko ndiko kunaleta makundi, alisimamia kwa haki na kupata watu kwa haki,” anasema.

Mwaselela anasema hakuna aliyepata nafasi kwa kubebwa, aliyekubalika alipata na ambaye hakukubalika hakushinda.

Mwaselela anasema kwa mara ya kwanza Rais Samia alisimamia uchaguzi huo kwa njia ya kunyooka, kwani aligundua baadhi ya watu waliingiza mizengwe iliyowagharimu, akalikataa hilo akisitiza mtu akakataliwe na wapigakura na si vinginevyo.

Uchaguzi Serikali za Mitaa

Mwaselela anasema CCM imejiandaa vizuri kwenda kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na katika uchaguzi huo, chama hakiwezi kuwadharau wapinzani, kwani hao wapo ili kuongeza ushindani, bila wao hata CCM haiwezi kuchangamka.

“Tunapaswa kujiandaa, sio kuwapuuza wapinzani, kufanya hivyo maana yake umeamua uchaguzi uje ili mpate shida, tunafahamu uchaguzi ni maandalizi na ni hesabu, ambacho tunakwenda kufanya ni kuleta wagombea wanaotokana na wananchi na wanaokubalika, lazima twende na sauti ya wananchi ili tufanye vizuri zaidi,” anasema.

Anasisitiza kwamba wakikubaliana na wananchi, wakawasimamisha wagombea wanaokubalika, hakuna neno upinzani litawasumbua.

“Tunataka mtu ambaye ni smart, tukimpeleka watu wamkubali, wananchi wao hii michakato ya ndani hawataki kuisikia, wanahitaji mgombea asiye na makandokando, anayekubalika, asiwe mwizi, sio mnaleta mgombea watu wanashangaa wanasema hadi huyu,” anasema.

Anasema yale malalamiko ya uchaguzi uliopita ya washindi kwenye kura za maoni kukatwa, safari hii wameyakataa, wanataka anayeshinda ashinde kihalali bila kuvunja kanuni na awe amezingatia miongozo na katiba ya chama.

“Wale wanaojipenyezapenyeza wanafahamu utaratibu ukoje? Atakayevunja taratibu vikao vya ngazi husika vitamwajibisha, tena mapema, habari ya kuvizia mtu amechukua fomu ndipo zinaletwa tuhuma zake hiyo haikubaliki,” anasema Mwaselela.

Kumekuwa na tetesi za kugawanywa kwa jimbo la Mbeya Mjini kwenye uchaguzi mkuu ujao, hata hivyo Mwaselela amekiri kwamba jambo hili lilikuwepo, lakini kwa sasa halipo baada ya Rais Samia kutoa ufafanuzi kwamba wajielekeze kwenye utoaji wa huduma.

Anasema maeneo mengi nchini walimuomba Rais Samia kugawa majimbo yaliyokuwa makubwa, yakiwemo ya Kawe, Segerea na mengine ya nje ya Dar es Salaam, ikiwamo la Mbeya Mjini, hata hivyo ameona hakuna umuhimu huo kwa sasa.

“Maelezo ya Rais ilikuwa kipaumbele cha sasa siyo kugawa majimbo, bali kuyahudumia, hivyo hadi sasa tumebaki na hayo maelekezo.

“Vilevile, kugawa maeneo huwa ni mkakati wa nchi na si kwa sababu ya kumlinda fulani, watu waondoe ile dhana kwamba jimbo likigawanywa ni sababu ya kumlinda fulani,” anasema.

Anasema ikitokea wakagawanywa kwa majimbo, ni kuwasha moto wa kisiasa, kwani watu wanaanza kujipanga.

“Kwa Mbeya Mjini, tunabaki na kauli ya Rais ya ‘sasa ni kuhudumia wananchi,’ kwani hata huko kwa wananchi tunapofanya ziara, wanachokiuliza ni lini barabara zitachongwa, umeme utafika hadi kwenye vitongoji, lini walimu wataongezeka? Na masuala ya maendeleo hawaulizi habari za kugawa jimbo,” anasema.

Related Posts