Fidia yaibua hofu kwa wananchi utekelezaji miradi

Unguja. Wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ikiendelea kutekeleza miradi ya maendeleo, ushirikishwaji hafifu wa wananchi na ulipaji fidia wa kusuasua ni miongoni mambo yanayolalamikiwa.

Baadhi ya miradi iliyotekelezwa na wananchi na kutakiwa kufidiwa, wanalalamika ulipaji umekuwa wa kusuasua.

Baadhi ya miradi inayolalamikiwa utoaji fidia ulichelewa ni  ujenzi wa barabara za mjini zenye urefu wa kilomita 100, ujenzi wa bohari ya Mangapwani, walioathiriwa na mtetemo wa utafutaji wa mafuta na gesi na ujenzi wa uwanja wa ndege Pemba.

Licha ya baadhi ya wananchi kufidiwa, inaelezwa fidia ilichukua muda mrefu.

Baadhi ya wananchi walioathiriwa na ujenzi wa uwanja wa ndege Pemba walilalamikia ucheleweshaji wa fidia licha ya tathimini kumalizika zaidi ya miaka miwili.

Bila kutaja kiasi kilicholipwa, katika hotuba ya Wizara ya Fedha na Mipango kwenye bajeti yake ya mwaka 2024/25 ilisema wananchi 744 wamelipwa fidia, huku wengine utaratibu wa kuwalipa ukiendelea.

Hoja ya ucheleweshaji wa fidia iliibuka katika mkutano wa 15 wa Baraza la Wawakilishi, baadhi ya wawakilishi waliitaka Serikali inapotekeleza miradi na kutwaa maeneo ya wananchi au kuharibu mazao yao iliwafidie mapema.

Mmoja wa wawakilishi hao, Suleiman Makame wa Jimbo la Ziwani amesema kutolipwa fidia kwa wananchi kunarejesha mipango yao nyuma kwani wamezuiwa kuendeleza maeneo yao kwa muda mrefu lakini hawapati mrejesho wowote.

Ucheleweshaji huo wa fidia hivi sasa umeibua hofu kwa wananchi wanaposikia katika maeneo yao kuna miradi inatakiwa kujengwa.

Matukio mawili ya hivi yanaonyesha hofu hiyo.

Hivi karibuni wananchi zaidi ya 400 wa Kijiji cha Paje Mkoa wa Kusini Unguja ambako Serikali inajipanga kujenga uwanja wa ndege.

Tukio lingine lililoibua hisia hizo ni la Chumbuni, Mkoa wa Mjini ambako Shirika la Nyumba la Zanzibar (ZHC) linatarajia kujenga nyumba zaidi ya 1,000 kwa ajili ya upangishaji.

Kutokana na wasiwasi walionao wananchi, watendaji wa Serikali wanalazimika kuzuru maeneo yao kuwatuliza kuhusu ushirikishwaji na ulipwaji wa fidia kwa wale watakaoathiriwa na miradi hiyo.

Wananchi zaidi ya 400 katika Kijiji cha Paje, Mkoa wa Kusini Unguja wameleza jinsi walivyopata tetesi za kutaka kuhamishwa kwenye maeneo yao kupisha ujenzi wa uwanja wa ndege bila kushirikishwa.

Kwa mujibu wa wananchi hao, wamekuwa wakiona wataalamu wanakwenda kupima maeneo yao lakini hawana taaarifa yoyote wala kushirikishwa.

Haji Nuru Said, mkazi wa eneo hilo amesema wao hawapingi mipango ya Serikali lakini wanachotaka ni ushirikishwaji ili watambue iwapo wakihamishwa wapi wanakwenda na ulipwaji wa fidia zao upoje.

“Kuna utata unaojitokeza watu wanakuja kupima kwenye maeneo yetu lakini hatuna taarifa na hatushirikishwi, tunaomba mchakato wote tushirikishwe na kujua kinachoendela,” amesema.

Kauli hiyo ilizungumzwa pia na Abubakar Mtumwa aliyesema: “Sisi hatupingi maendeleo lakini tunasikia huko tu, hatushirikishwi kwenye hatua zote ili kuridhia au kama tutatakiwa kuondoka tujue ni wapi tunakwenda na katika misingi gani.”

Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Dk Khalid Salum Mohamed amelazimika kwenda kijijini hapo kukutana na wananchi kutoa ufafanuzi kuhusu kinachoendelea.

Dk Khalid amesema Serikali haiwezi kufanya uamuzi bila kuwashirikisha wananchi wa eneo husika.

Amesema bado mchakato wa ujenzi wa uwanja huo upo kwenye hatua za awali kwa hiyo iwapo kukiwa na uamuzi wa kujenga uwanja huo lazima wananchi hao watashirikishwa na ikiwezekana hata watakaotakiwa kupisha watalipwa fidia.

“Serikali haiwezi kufanya jambo bila kuwashirikisha na hakuna mwananchi atakayeondolewa kwenye eneo lake, kinachofanyika kwa sasa bado ni upembuzi yakinifu, iwapo uamuzi ukifikiwa kila kitu kitakuwa sawa,” amesema Dk Khalid.

Kwa sasa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina mpango wa kujenga viwanja vya ndege katika maeneo yenye kuvutia utalii kwa kasi ili kurahisisha kufikika ikiwa ni pamoja na Paje, Mkoa wa Kusini Unguja na Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Kama ilivyotokea kwa wananchi wa Kijiji cha Paje, hali hiyo imejitokeza katika eneo la Chumbuni, Mkoa wa Mjini ambako Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC) linatarajia kujenga nyumba za biashara.

Mradi huo wa nyumba 1,095 umeibua hofu kwa wananchi wa eneo hilo, wakitaka kuwapo ushirikishwaji na kupewa utaratibu wa malipo ya fidia kwa wale watakaoathiriwa na mradi huo, kwa kuwa eneo hilo ni maarufu kwa kilimo.

Wakizungumza wakati wa mkutano wa kutoa maoni kati yao na watendaji wa Serikali Julai 16, 2024, wananchi hao akiwamo Talib Mohamed Bakari wameoimba Serikali kuwatambua wananachi wenye mazao katika eneo hilo.

Wametaka kufanyika tathmini na kuhakikisha kila mwananchi analipwa fidia.

“Tunaomba Serikali itafute namna ya kulipa fidia au kutupatia makazi ya kuishi baada ya mradi wa nyumba hizi kukamilika,” amesema Talib Mohamed, mkazi wa eneo hilo.

Sada Juma Vuai, amewasihi viongozi kutekeleza ahadi wanazotoa katika kipindi cha kupisha ujenzi wa mradi huo, akidai kumekuwapo changamoto kwenye maeneo mengine wananchi kucheleweshewa malipo ya fidia.

Akizunguzia hilo, Mkurugenzi Mkuu wa ZHC, Sultan Said Suleiman amesema ujenzi  hautaathiri makazi ya watu badala yake mazao (vipando) vilivyopo katika eneo hilo ndivyo vitakavyoathirika na watakaoathiriwa watafidiwa.

Amewataka wananchi kufika kwenye ofisi za viongozi wa shehia kuhakikisha kila aliye na vipando anapata fidia yake.

“Nawaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa kampuni itakayopewa jukumu ili kufanikisha mradi huu utakaosaidia kupata makazi bora na salama,” amesema Sultan.

Naibu Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Salha Mohammed Mwijuma amesema ujenzi huo utasaidia juhudi za Serikali za kuleta mageuzi ya makazi.

Amesema mradi huo ni miongoni mwa utekelezaji wa ahadi za Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi katika kuhakikisha miji inaimarika na wananchi wanakuwa na makazi bora na salama.

Amewataka wananchi kuwa walinzi na wasimamizi wa rasilimali za ujenzi huo ili lengo lifikiwe.

“Naomba msisite kutoa taarifa za changamoto zitakazojitokeza wakati mradi unaendelea kwa lengo la kutatuliwa na kufanya mradi huo kukamilika kama ilivyokusudiwa,” amesema Salha.

Amesema wameshakubaliana na wakandarasi wa ujenzi huo kutoa kipaumbele cha ajira kwa vijana wenyeji wa jimbo hilo.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi na Makazi Zanzibar, Mhaza Gharib Juma amesema mbali na nyumba hizo, mradi  utazalisha ajira 1,500 zitakazowanufaisha wananchi wa jimbo hilo.

Mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi Chumbuni utasimamiwa na kampuni ya Wehian Hutan Ltd kutoka China na unatarajiwa kuchukua miezi 14 hadi kukamilika.

Related Posts