Greenwood mambo freshi Marseille | Mwanaspoti

MARSEILLE, UFARANSA:KLABU ya Marseille imefikia makubaliano na Mason Greenwood kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji huyo kutoka kwa miamba ya Ligi Kuu England, Manchester United.

Klabu hizo mbili zilishafikia makubaliano ya ada ya awali ya uhamisho ya Pauni 27 milioni pamoja na Pauni 3.2 milioni za ziada kwa ajili ya kumsajili Greenwood, lakini zilihitaji pia ridhaa ya fundi huyo mwenye umri wa miaka 22 ili dili hilo litimie.

Na sasa maafikiano ya mdomo yamefikiwa kati ya mchezaji na klabu hizo mbili kuhusu uhamisho huo, lakini dili bado halijakamilishwa.

Greenwood ni lazima kwanza asafiri kwenda Ufaransa kufanyiwa vipimo vya afya na asaini nyaraka muhimu kabla ya dili hilo kutangazwa kuwa limekamilika.

Uhamisho wake wa kwenda Marseille utamfanya Greenwood kwenda kucheza chini ya kocha Roberto De Zerbi, ambaye aliteuliwa kuifundisha miamba hiyo ya Ligue 1 mwezi Juni.

Hata hivyo, baadhi ya mashabiki wa Marseille wameanzisha kampeni ya #GreenwoodHakaribishwi kutokana na tuhuma za jaribio la kubaka na mashitaka ya shambulio yaliyomkabili mchezaji huyo Muingereza.

Meya wa Jiji la Marseille, Benoit Payan pia anapinga uhamisho huo, akisema atamshawishi rais wa klabu hiyo Pablo Longoria kuachana na usajili huo.

Hata hivyo, Greenwood alikana kufanya kosa lolote na mashitaka yote yalifutwa na mahakama ya Crown mwaka jana.

Licha ya vikwazo hivyo, Greenwood amedhamiria kupambana kuhakikisha dili hilo linafanikiwa.

Alirejea mazoezini Man United Jumatatu na akazungumza na uongozi wa timu kuhusu kuondoka Old Trafford.

Greenwood hajaichezea Man United tangu Januari 2022 pale tuhuma hizo zilipoibuliwa.

Related Posts