MBIO za magari nchini Hungary wikiendi hii zinatarajiwa kuwa na msisimko wa aina yake kutokana na kampuni ya Mercedes kushinda mbili mfululizo zilizopita nchini Austria na Uingereza.
Madereva George Russell na Lewis Hamilton ndio waliofanikisha ushindi huo ambao umeirudisha kwenye chati kampuni hiyo kiasi cha kuamsha vita mpya kati ya kampuni hizo pinzani kwa miaka mitano sasa, huku upinzani ukikolea zaidi.
Hungary inakwenda kuwaka moto pale kampuni hizo zinapotarajia madereva wao washinde huku kukiwa na moto wa McLaren kupitia Lando Norris ambaye amekuwa karibu kutoa upinzani kwa bingwa Max Verstappen wa Red Bull.
Hali hiyo inafanya mbio za Hungary ziwe na msisimko mkubwa kwani madereva wanne tofauti wameshinda zilizopita kuanzia Norris, Verstappen, Russell na Hamilton kuwa kwenye vita kali ya kila mmoja kuitaka mbio hiyo ili kuongeza alama za kuwania taji la dunia, mwaka huu.