Kilolo wahakikishiwa kiwanda cha sukari, watenga hekta 17 kulima miwa

Iringa. Wananchi wa Kata ya Nyanzwa wilayani Kilolo mkoani Iringa, wametenga hekta 17 kwa ajili ya kilimo cha miwa baada ya kuhakikishiwa uwekezaji wa kiwanda cha sukari.

Diwani wa Nyanzwa, Boniface Mgwale amesema mbali na kutenga hekta 17, kila mwananchi wa kata hiyo yupo tayari kutenga shamba kwa ajili ya kilimo cha miwa kama fursa mpya ya kiuchumi kwenye eneo lao.

“Tumezoea kulima vitunguu na nyanya, lakini kwa fursa hii tuliyopata, sasa tupo tayari kuanza kilimo kipya cha miwa, tunachosubiri ni kujengwa kwa hicho kiwanda tu,” amesema Diwani Mgwale.

Naye mkulima wa vitunguu katika eneo hilo, John Msangawale amesema licha ya kubobea kwenye kilimo cha vitunguu, huu ni wakati wake wa kuongeza kulima zao lingine la biashara la miwa.

“Ardhi ninayo, Serikali inasema inajenga kiwanda cha sukari na mimi ninaanza kulima miwa niongeze eneo lingine la kupata mafanikio,” amesema Msangawale.

Marry Isagito makazi wa Kijiji cha Nyanzwa amesema awali walikuwa wanategemea zaidi mazao ya nyanya, vitunguu, mahindi na maharage na sasa wataongeza na kilimo cha miwa.

Amesema wakiwa na kiwanda hicho cha sukari, mbali ya fursa ya kilimo cha miwa, lakini pia ajira zitaongezeka.

Akizungumza na Mwananchi, mbunge wa Kilolo, Justine Nyamoga amesema kwa sababu tayari mchakato wa uwekezaji wa kiwanda umeanza, wananchi wameshajiandaa kwa ajili ya kiwanda hicho.

Amesema hekta hizo zitafaa kwa kilimo na uwekezaji wa kiwanda cha sukari.

“Nimefuatilia na mchakato umeanza kwa hiyo sisi wana Kilolo tumeshatenga ardhi kwa ajili ya kilimo hiki kipya kwenye wilaya yetu,” amesema Nyamoga na kuongeza:

“Niwaombe wananchi msiuze maeneo yenu kiholela kwa sababu tukisema ujenzi wa kiwanda upo, mjue watu wengi watakuja huku, kuliko tubaki watumwa wa kufanya vibarua, basi tubaki na mashamba yetu,” amesema mbunge huyo.

Related Posts