KONA YA MALOTO: Tukio la Trump linathibitisha Marekani ni ileile

John Hinckley Jr, alitekwa kihisia na mwigizaji wa Hollywood, binti mrembo, Jodie Foster. Filamu ya Taxi Driver ilipotoka mwaka 1976, Hinckley, angeitazama kila siku ili kumwona Jodie. Hinckley alimpenda sana Jodie. Haukuwa upendo wa kawaida, bali ugonjwa.

Hinckley alifanya majaribio mengi ya kumsogeza Jodie karibu. Alimwandikia barua mara kwa mara. Mara chache alizungumza naye kwa simu. Hinckley alipogundua Jodie hakuwa na mpango naye, akawaza nini afanye ili kuziteka hisia za mrembo huyo? Mwisho kabisa, Hinckley akapata jibu kwamba endapo angemuua rais, angekuwa maarufu, kisha Jodie angevutiwa naye, kwani wangekuwa sawa kwa umaarufu.

Uchaguzi wa Rais Marekani 1980, Hinckley, alisafiri jimbo kwa jimbo akiufuata msafara wa Rais Jimmy Carter, aliyekuwa anawania urais kwa muhula wa pili kwa tiketi ya chama cha Democratic, dhidi ya Ronald Reagan, aliyesimama kwa leseni ya Republican. Rais Carter, alipofanya kampeni zake Dayton, Ohio, Hinckley alimsogelea kwa umbali wa futi 20. Akaona kumbe ni rahisi kumfikia.

Oktoba 9, 1980, Hinckley, aliyekuwa na umri wa miaka 25, aliingia Nashville, Tennessee, siku ambayo Carter pia alikuwa na ziara kwenye jiji hilo. Hinckley, alikamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Nashville, akiwa na bunduki tatu kwenye begi. Alitozwa faini ya dola 50 na gharama za mahakama, kwa kumiliki bunduki isivyo halali. Alinyang’anywa bunduki. Hinckley alikamatwa akiwa anataka kupanda ndege kwenda New York, kuufuata msafara wa Carter. Polisi hawakujua kuwa zile bunduki, Hinckley alilenga kuzitumia kumuua Rais Carter.

Baada ya kuachiwa huru Nashville, Oktoba 13, 1980, Hinckley alisafiri mpaka nyumbani kwao, Dallas, Texas, alikonunua bastola aina ya Rohm RG 14. Mizunguko yote hiyo, Hinckley aliifanya baada ya kuwaibia wazazi wake dola 3,600. Zote ziliisha. Alirudi nyumbani mikono mitupu. Uchaguzi ulifanyika Novemba 4, 1980. Reagan alimshinda Carter. Hinckley akabadili malengo, shabaha yake ikawa Reagan. Akaanza kujifunza jinsi Rais John Kennedy, alivyouawa Novemba 22, 1963.

Machi 29, 1981, Hinckley aliwasili Washington DC, akitokea Los Angeles kwa basi. Alipitisha usiku wake hotelini. Asubuhi, Machi 30, 1981, Hinckley alimwandikia barua Jodie, akimweleza kuwa anaelekea kumpiga risasi Rais Reagan kwa sababu jitihada zake za kumvutia kwa maneno na mashairi zilishindikana. Siku hiyo, Hinckley, alikuwa mmoja waliohudhuria mkutano wa Reagan na shirikisho la wafanyakazi, uliofanyika Hoteli ya Hilton, Washington DC.

Mkutano ulipokamilika, Rais Reagan akiwa anarejea kwenye gari lake, Hinckley alichomoa bastola yake, Rohm RG 14, akafyatua risasi zote sita zilizokuwemo. Risasi ya kwanza ilimjeruhi msaidizi wa Rais Reagan wa masuala ya habari, James Brady, ya pili ilimpiga askari polisi, Thomas Delahanty, ya tatu haikumpiga mtu, ila ya nne, ilimjeruhi ofisa usalama wa Secret Service, Timothy McCarthy, ambaye alisimama kumkinga Rais Reagan. Risasi ya tano iligonga kioo cha gari chenye kuzuia risasi, ya sita ndiyo ilimpiga Reagan na kumjeruhi vibaya kifuani.

Baada ya tukio hilo, Hinckley alikamatwa, Reagan alihifadhiwa hospitali kwenye wodi ya uangalizi maalumu (ICU).

Imepita miaka 43 tangu shambulizi la Reagan, Rais wa 45 wa Marekani, Donald Trump, akiwa kwenye kampeni ya kurejea kwenye kiti cha urais, baada ya kushindwa Uchaguzi wa Rais 2020, naye ameshambuliwa. Ni nusura kwake risasi ilimparaza sikioni na kumjeruhi kidogo.

Ilikuwa Pennsylvania, katikati ya mkutano wa kampeni, kijana Thomas Mattew Crooks, alifyatua risasi kumwelekea Trump. Mtu mmoja alifariki dunia, wengine walijeruhiwa. Crooks naye aliuawa baada ya kupigwa risasi na maofisa usalama, kitengo cha ulinzi wa viongozi Marekani (Secret Service). Kila mtu anaalani tukio hilo, kuanzia Rais Joe Biden, ambaye anashindana na Trump uchaguzi wa Novemba 2024, hadi jumuiya zote za usalama.

Nadharia mbalimbali zimesemwa. Kuna wanaodai risasi ya Trump ni mpango wa kutafuta mavuno ya huruma kuelekea uchaguzi. Wengine wanadai Trump anavuna upandaji wake wa misimamo na hotuba za chuki. Wapo wanaodhani ni mpango wa mataifa hasimu kuichonganisha nchi hiyo, maana Uchaguzi wa Rais 2024 unabeba hisia kali na kuigawa nchi katikati. Kuuawa kwa Trump kungetengeneza hasira kali kwa wafuasi wake.

Kuna wanaodhani Trump amenufaika kwa shambulizi hilo, maana wengi watamhurumia kuelekea uchaguzi. Wengine wanaona shambulio la Trump limempa ahueni Biden, ambaye anakabiliwa na presha kubwa ndani ya chama chake. Kuna kundi kubwa, wakiwemo maseneta na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wanataka Biden ajitoe kwenye mbio za uchaguzi ili chama cha Democrat, kitafute mgombea mwingine. Tangu shambulizi la Trump, presha dhidi ya Biden imepungua. Hisia zote zipo kwa Trump.

Ukiweka pembeni hayo, ukweli ni kuwa shambulizi dhidi ya Trump linathibitisha Marekani ni ileile yenye ghasia na vurugu, ingawa kwa nje hupambwa kama taifa lenye ustaarabu mkubwa. Marekani ni ileile ambayo marais wake wanne waliuawa kwa risasi wakiwa madarakani; Abrahm Lincoln (mwaka 1865), James Garfield (mwaka 1881), William McKinley (1901) na Kennedy.

Ni Marekani ambayo marais wake watatu wakiwa madarakani, wamejeruhiwa kwa risasi; Reagan, Theodore Roosevelt (mwaka 1912) na Trump. Tangu Bunge la Marekani lilipoanzishwa Machi 4, 1789, kwa maana ya chemba zote mbili, Seneti na Baraza la Wawakilishi, jumla ya wabunge (maseneta na wajumbe wa baraza) 15 wameshauwa, 14 wakijeruhiwa vibaya. Jumla ni 29.

Jenga mifano kupitia majaribio ya kuuawa ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Gabrielle Giffords, mwaka 2012, Steve Scalise (2017) hadi Angie Craig (2023), utaona kuwa Marekani ni ileile yenye ghasia, ila hupambwa utadhani ndilo taifa salama kuliko yote ulimwenguni. Mtandao wa The Trace, umeonyesha kuwa mwaka 2023 pekee, vifo vitokanavyo na bunduki Marekani ni 18,874, waliojeruhiwa ni 36,357, wakati watoto waliopigwa risasi mwaka 2023 ni 6,192.

Dunia huonyeshwa kuwa magenge hatari na upatikanaji holela wa bunduki, vimeshamiri nchi za Latini Amerika. Ukweli ni kuwa Marekani ndiyo dampo la magenge ya dawa za kulevya, mafia, bunduki zipo njenje, kiasi kwamba mtu akitaka kutekeleza mpango wake wa mauji, hahangaiki kupata silaha. Marekani ni sawa na mwili mchafu, unaopuliziwa manukato kukata shombo, kisha unavalishwa suti nadhifu upendeze. Ni sawa na ngano ya uzuri wa ukakasi ndani kipande cha mti.

Related Posts