Kupotea kwa muuguzi KCMC bado giza nene

Moshi. Zikiwa zimepita siku 16  tangu kutoweka kwa muuguzi wa Hospitali ya KCMC, Lenga Masunga (38), Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema  bado wanaendelea na uchunguzi.

Muuguzi huyo wa idara ya masikio, pua na koo anadaiwa kutoweka katika mazingira ya kutatanisha Julai 2, mwaka huu nyumbani kwake Mtaa wa Rau Pangaleni, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro alikokuwa akiishi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Hospitali ya KCMC, Masunga alikuwa mapumziko ya siku mbili, Julai 2 na 3 na alitakiwa kuwepo kazini Julai 4, mwaka huu, lakini hakuonekana hali ambayo iliibua mashaka na kuufanya uongozi wa hospitali hiyo kuanza kumtafuta kupitia simu zake za mkononi ambazo hazikupatikana mpaka sasa.

Kamanda Maigwa amesema wanaendelea na uchunguzi wa kutoweka kwa muuguzi huyo kwa kushirikiana na uongozi wa hospitali hiyo na tayari wameshamuhoji mchumba wa muuguzi huyo pamoja na mwenye nyumba alikokuwa amepanga.

“Huyu muuguzi alitakiwa arudi kazini Julai 4, mwaka huu lakini hakuonekana tangu tarehe hiyo, tunaendelea kufuatilia kwa sababu hata simu zake hazipatikani,” amesema RPC Maigwa na kuongeza;

Kaka wa muuguzi huyo, Paschal Jeremiah ameiomba Serikali kuongeza nguvu ya kumtafuta ndugu yao kwa kuwa wanakosa amani.

“Tunaiomba Serikali itusaidie kupitia vyombo vyake vya dola kuchunguza, wazazi hawalali ndugu tunahaha usiku na mchana lakini hatujui huyu ndugu yetu amekumbwa na nini, maana mpaka leo simu zake hazipatikani,” amesema Jeremiah.

Masunga ambaye alikuwa amtolee mahari mchumba wake, Neema Mmasy mwezi huu, alitoweka nyumbani kwake katika mazingira ya kutatanisha na kuacha nyumba aliyokuwa akiishi ikiwa wazi huku baadhi ya vitu vyake yakiwamo mabegi ya nguo yakiwa yamepekuliwa.

Related Posts