Arusha. Mahakama ya rufani imebariki adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela aliyohukumiwa mkazi wa Wilaya ya Ngorongoro, Paryumbai Kishando, baada ya kutiwa hatiani kwa kukutwa na meno mazima manne na vipande viwili vya meno ya tembo na ngozi ya chui.
Rufaa hiyo ilikuwa inapinga uamuzi wa Mahakama Kuu Masijala ndogo ya Arusha, iliyotolewa Februari 17,2021.
Katika kesi hiyo, Paryumbai alishtakiwa kwa makosa mawili ya kukutwa na nyara ya Serikali ambayo ni meno manne na vipande viwili vya meno ya tembo na ngozi ya chui kinyume na kifungu cha 86 (1) (2) (b) na (3) cha Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009 kama ilivyorekebishwa mwaka 2016.
Kifungu hicho kilisomwa pamoja na aya ya 14 (d) jedwali la kwanza na kifungu cha 57 (1) na 60 (2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupanga, Sura ya 200 (EOCCA).
Hukumu hiyo ilitolewa Jumatatu Julai 15, 2024 na Mahakama ya Rufani iliyoketi Arusha mbele ya jopo la majaji watatu wakiongozwa na Mwenyekiti wake Stella Mugasha, Dk Mary Levira na Omar Othman Makungu.
Kwa mujibu wa kumbukumbu za Mahakama, katika mashitaka yote mawili, inadaiwa Oktoba 24, 2016 katika Kijiji cha Mhoro Wilayani Ngorongoro mkoani Arusha, Kishando alikutwa na meno hayo yenye thamani ya Dola 60,000 za Marekani (zaidi ya Sh131.16 milioni) na ngozi moja ya chui yenye thamani ya Dola 3,500 za Marekani (zaidi ya Sh7.65 milioni).
Ilidaiwa Kishando alikutwa na mali hizo za Serikali bila kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Ili kuthibitisha kosa hilo, upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi wanne na vielelezo saba.
Shahidi wa pili upande wa mashitaka, Melkiori Mtui ambaye ni Askari wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, alidai mahakamani hapo kuwa walipata taarifa kutoka kwa raia mwema kwamba kuna watu wanatafuta mnunuzi wa meno ya tembo, hivyo wanataka aunganishwe nao.
Alidai walipanga mtego ambao wanunuzi watarajiwa walikubaliana na wauza akiwamo mrufani, kukutana eneo la msituni.
Ambapo wauzaji hao walifika eneo hilo kutokea msituni wakiwa na mifuko miwili iliyokuwa na nyara hizo za Serikali.
Shahidi huyo alidai washukiwa walipoingia kwenye gari, walikamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi Ngorongoro.
Shahidi wa nne, alidai Oktoba 25, 2016 alichunguza, kuthamini na kupima nyara hizo kisha alirekodi maelezo ya onyo ya mrufani yanayoonyesha alikiri makosa hayo.
Akijitetea mahakamani hapo, Kishando alidai hakukamatwa Oktoba 22, 2016 akiwa Ololosokwan, Loliondo bali alikamatwa alipokuwa kwenye mnada akiuza ng’ombe kwa tuhuma za wizi wa mifugo akiwa na wenzake wawili.
Alidai tangu walipokamatwa, walikaa kituoni kuanzia Oktoba 22 hadi Novemba 7,2016 na walipigwa na kulazimishwa kusaini cheti cha kukamata, kielelezo na maelezo ya onyo.
Kwa mujibu wa kumbukumbu hizo, Jaji Mugasha aliridhika kwamba mrufani alikamatwa kisheria kwa kosa la kukutwa na nyara za Serikali na adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela ni halali.
Mrufani huyo aliwakilishwa na mawakili wawili akiwemo Fridolin Bwemelo aliyetoa sababu tano za kukata rufaa.
Alidai kuwa mashauri ya Mahakama yamegubikwa na ukiukwaji mkubwa wa taratibu usioweza kutibika ambao unafanya uamuzi wake wote kuwa batili.
Sababu nyingine, Bwemelo alidai kuwa Mahakama ilikosea kisheria kushughulikia ushahidi wa upande wa mashitaka pekee, pasi kuzingatia ushahidi wa utetezi.
“Lakini pia Mahakama imeshindwa kutathmini ushahidi ipasavyo na kesi ya mashitaka haikuthibitishwa bila kuacha shaka yoyote,” alidai Bwemelo.
Lakini pia Wakili Bwemelo alidai hakukuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kilichotolewa baada ya shitaka hilo kufanyiwa marekebisho na kubadilishwa.
Alidai baada ya marekebisho ya Februari 9, 2021 ya shitaka la awali ambalo lilikuwa na ridhaa na cheti cha kuwaruhusu washitakiwa wawili kuhukumiwa na Mahakama ya Mwanzo na kumuacha mshitakiwa wa pili, hakuna ridhaa mpya ya kumsikiliza mrufani hivyo aliomba rufaa hiyo ikubaliwe.
Akizungumzia hoja ya utetezi wa mrufani kutozingatiwa, wakili huyo alidai kuna mkanganyiko wa ushahidi wa upande wa mashitaka kuhusiana na eneo alilokamatwa mrufani ambalo ni Mhoro, Muhuro au Kijiji cha Mholo na kuwa katika utetezi, mrufani alieleza kwamba alikamatiwa Ololosokwan.
Akijibu hoja hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Lilian Kowero na wenzake wawili alikubali shitaka lilibadilishwa ila ridhaa iliyo katika ukurasa wa 77 wa rekodi ya rufaa ilikuwa halali kuipa mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Alidai kubadilishwa kwa shitaka baada ya kumwondoa mshtakiwa wa pili, hakuondoi mamlaka ya mahakama.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Jaji Makungu alisema wanakubali kwamba shitaka la awali linalowahusisha washtakiwa wawili lililowasilishwa Novemba 25, 2016, lilikuwa na kibali chake na iliipa mahakama ya awali mamlaka ya kusikiliza makosa ya kiuchumi.
Alisema Februari 9, 2021, shitaka lilibadilishwa na mshtakiwa wa pili aliondolewa na likabaki kwa mrufani pekee.
Alifafanua kumuondoa mshtakiwa wa kwanza, hakuondoi mamlaka ya Mahakama ya awali kuhusiana na mrufani.
Jaji alisema kutokana na kuzingatia mazingira ya kesi hiyo, wamebaini kushindwa kutoa ridhaa mpya baada ya kubadilisha shitaka kwa kumuondoa mshtakiwa wa pili, hakukuwa na haja ya idhini mpya, hivyo hoja hiyo ya kukata rufaa haina mashiko na kuitupilia mbali.
Jaji Makungu alisema kuhusu hoja ya upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha makosa hayo pasipo shaka, wamekubaliana na wakili Kowero kwamba makosa hayo yalithibitishwa pasipo shaka yoyote.
Baada ya kupitia hoja zote za rufaa, Jaji Makungu alisema kwa ushahidi katika rekodi ya rufaa, wameridhika kwamba makosa yalithibitishwa bila shaka dhidi ya mrufani, hivyo kutupilia mbali rufaa hiyo akisema haina mashiko.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.