Masasi. Miili ya mapadri wawili na bruda mmoja wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mtwara, waliofariki dunia kwa ajali ya gari Ijumaa Julai 12, 2024, imezikwa leo katika makaburi ya Kanisa la Mtakatifu Benedictine Abasia ya Ndanda, Jimbo Katoliki la Mtwara, huku Askofu Wolfgang Pisa akilia na ubovu wa barabara mikoa ya kusini.
Ajali hiyo iliyokatisha uhai wa watumishi hao wa Mungu ilitokea eneo la Mtualonga, barabara ya Masasi- Mnazi mmoja katika Halmsahauri ya Mtama mkoani Lindi.
Julai 12, 2024, akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, John Imori alisema gari walilokuwa wakisafiria viongozi hao wa dini aina ya Mistubish Outlander, iligonga shimo na kupoteza uelekeo kabla ya kwenda kugonga karavati na kuingia kwenye shimo na kusababisha vifo vya mapadri hao wawili na bruda mmoja, huku wengine wawili wakijeruhiwa.
Aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Bruda Bakanja Mkenda (51), Padri Pius Boa (51) na Padri Cornelius Mdoe (55).
Maziko hayo yalitanguliwa na Ibada Takatifu ya kuwaombea marehemu hao iliyoanza saa mbili asubuhi na kukamilika saa 8:00 mchana.
Akizungumza katika ibada ya maziko hayo leo Jumatano Julai 17, 2024, Askofu Wolfgang Pisa wa Jimbo Katoliki Lindi na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), ameiomba Serikali itengeneze Barabara ya Masasi – Mnazi mmoja ambayo ina mashimo mengi, ili kuepusha ajali zinazotokea mara kwa mara na kugharimu maisha ya watu.
Amesema baada ya mvua kubwa kunyesha zilizoambatana na kimbunga Hidaya, barabara hiyo imezidi kuharibika na hivyo kuhitaji ukarabati mkubwa.
“Barabara yetu hii ya kusini imeharibika sana, kuanzia Rufiji, Somanga, Matandu na Mbwemkuru kutokana na mvua kubwa iliyonyesha ikiambatana na kimbunga Hidaya, niiombe Serikali itusaidie kuboresha barabara hiyo, ili tuepushe ajali hizi.
“Shimo lililokuwa barabarani limesababisha vifo vya mapadri wetu wawili na mtawa huyo. Niiombe sana Serikali, ione namna ya haraka ya kuifanyia ukarabati barabara hii,” amesema Askofu Pisa na kuongeza;
“Chanzo cha ajali hii ni shimo na hadi leo bado lipo halijafanyiwa ukarabati, niwaombe wenye mamlaka pia wajitahidi kuweka alama za barabarani, ili iwe rahisi kwa dereva kujua mbele yake kuna tatizo kwenye barabara.”
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala amesema barabara ya kutoka Mtwara hadi Masasi imeshafanyiwa upembuzi yakinifu na wakati wowote ujenzi utaanza.
“Zaidi ya kilomita 200 zimeshafanyiwa upembuzi yakinifu kutoka mkoani Mtwara hadi Masasi kwa kupitia barabara ya Mnazi mmoja na eneo ilipotokea ajali pia patajengwa, Serikali imeshatenga fedha tunasubiri utekelezaji tu,” amesema Kanali Sawala.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.