Mawakili 29 kumtetea Mwabukusi Mahakama Kuu 

Dar es Saaam. Mawakili 29 wa kujitegemea wanatarajia kumtetea wakili Boniface Mwabukusi katika shauri la maombi Mahakama Kuu anayoiomba kufanya marejeo ya uamuzi uliomwengua kwenye orodha ya wagombea urais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

Mawakili hao wanaongozwa na Mpare Mpoki, akisaidiana na Jebra Kambole, John Malya anayemwakilisha Pater Kibatala, Dickson Matata, Edward Heche na Ferdinand Makore.

Mpoki ameieleza Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, leo Julai 17, 2024, Mbele ya Jaji Mfawidhi wa mahakama hiyo, Salma Maghimbi.

Upande wa wajibu maombi ambao ni TLS wanawakilishwa na Wakili Steven Mwakiborwa na Hekima Mwasipu.

Awali, shauri hilo lilipoitwa mahakamani, Mpoki aliieleza Mahakama lilipangwa kutajwa na upande wa wajibu maombi wamekubali kuwa wamepokea nyaraka.

Jaji Maghimbi baada ya kusikiliza hoja hizo, ameahirisha kwa muda shauri hilo hadi mchana wa leo Julai 17, 2024.

Mwabukusi alifungua shauri hilo Julai 11, 2024 katika Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.

Wakili huyo alikuwa miongoni mwa wagombea sita waliopitishwa na Kamati ya Uchaguzi ya TLS kugombea nafasi hiyo Juni 24, 2024.

Wagombea wengine waliopitishwa kuwania urais katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Agosti 2, jijini Dodoma ni Ibrahim Bendera, Emmanuel Muga, Revocatus Kuuli, Paul Kaunda, na Sweetbert Nkuba.

Ikielezwa ni kwa sababu ya doa la kimaadili, Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi TLS ilimuengua Mwakubusi kwenye kinyanganyiro hicho kitendo anachokipinga.

Mwabukusi anaiomba mahakama kufanya marejeo akidai Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TLS imemuengua pasipo kumpa nafasi ya kusikilizwa.

Anadai kulikuwa na ukiukwaji wa haki za binadamu na haki ya asili kwa kutoa hukumu bila kumshirikisha.

Related Posts