Msimamizi wanafunzi Mirerani adaiwa kujinyonga shuleni kwa kamba

Mirerani. Msimamizi wa Shule ya Awali na Msingi New Vision,  mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara, amedaiwa kujinyonga kwa kutumia kamba ya manila.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP), George Katabazi akizungumza leo Jumanne Julai 16 2024 amemtaja msimamizi huyo kuwa ni Paulo Essau (32) mkazi wa Kitongoji cha Songambele.

Kamanda Katabazi amedai kuwa Essau amefariki dunia kwa kujinyonga akiwa ndani ya ghala la kuhifadhi chakula cha shule hiyo.

“Essau alijinyonga kwenye stoo ya kuhifadhi mahindi ya shule hiyo kwa kutumia kamba aina ya manila na akafariki dunia papo hapo,” amedai.

Amesema tukio hilo lilitokea Julai 14 2024 saa 10 jioni baada ya mwangalizi wa watoto wa shule hiyo, Paulo Essau kuukuta mwili wa mwalimu huyo ukiwa unaning’inia kwenye ghala hilo.

Amesema bado hawajabaini chanzo cha tukio hilo na polisi wanaendelea na uchunguzi.

Amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa kwenye chumba cha maiti cha Kituo cha Afya Mirerani.

Mkurugenzi wa Shule ya New Vision, Prisca Msuya amedai hafahamu chanzo cha kifo hicho cha msimamizi huyo kujinyonga.

Amesema msimamizi huyo alikuwa amekwenda nyumbani kwao hivi karibuni na kurejea baada ya wiki moja.

“Alikuwa mpweke mno kila wakati ni mkimya na akiulizwa hajibu kitu chochote kile mara nyingi akawa amejitenga ya peke yake bila kuwa na mtu,” amesema.

Amesema ingelikuwa vyema endapo angezungumza chochote kinachomsibu ila alikuwa hazungumzi na ndipo alipochukua uamuzi huo.

Amesema bado wanawasubiria ndugu wa marehemu ambao ndiyo wataamua taratibu za maziko zitakavyokuwa.

Mmoja kati ya walimu wa shule hiyo ambaye hakutaka kutaja jila lake amesema hawajajua chanzo cha kifo hicho kwa kujinyonga kwa kuwa hakuwa na ugomvi na mtu shuleni hapo.

Tumelazimika kufanya masahihisho katika habari hii kutokana na tatizo la kiufundi. Katika habari tuliyochapisha awali ilimtambulisha mwalimu John Msinga (34) kama ndiye aliyejinyonga. Usahihi aliyejinyonga ni msimamizi wa wanafunzi katika shule hiyo, Paul Essau (32) na sio John.

Tunaomba radhi kwa John binafsi, uongozi wa shule, familia yake na wasomaji wetu kwa usumbufu uliojitokeza.

Related Posts