Timu ya Wanawake ya Brighton ya England imetangaza kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Aisha Masaka kutoka BK Hacken ya Sweden kwa mkataba ambao haujawekwa wazi.
Mkurugenzi wa Soka la Wanawake wa timu hiyo, Zoe Johnson amesema “Tuna furaha sana kumkaribisha Aisha hapa Brighton, amekuwa kwenye kiwango cha juu huko Sweden akiitumikia Hacken kwenye Ligi ya Mabingwa barani Ulaya, Yeye ni mshambuliaji ambaye anatawala mpira na mfungaji wa asili”
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20 alijiunga na Hacken mwaka 2022 akitokea Young Africans ya Tanzania, akiwa amewahi kuichezea Alliance FC ya Mwanza
Katika misimu miwili aliyokaa Hacken, Mshambuliaji huyo aliwasaidia kumaliza nafasi ya pili kwenye Ligi ya Sweden na walifika robo fainali ya UEFA Champions League msimu uliopita kabla ya kufungwa na PSG.
Akiitumikia Ligi Kuu ya Tanzania Aisha alishinda kiatu cha ufungaji bora katika kampeni za 2020/21 baada ya kuifungia Young Africans mabao 35 katika mechi 20 huku akiwa ameitumikia Timu ya taifa ya Tanzania katika mechi 15, akifunga mabao tisa tangu alipoanza kuitumikia Tanzania mwaka 2021.