Niyonzima arejea Rayon Sport | Mwanaspoti

Kiungo mkongwe Haruna Niyonzima amerejea nchini kwao Rwanda baada ya kusaini mkataba na timu yake ya zamani ya Rayon Sport.

Niyonzima, amesaini mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongeza mwaka mwingine kuitumikia Rayon.

Hii inakuwa ni mara ya pili kwa Niyonzima kufanya kazi na Rayon, ambayo aliwahi kuitumikia msimu wa 2006-2007.

Tayari Rayon, imeshamtambulisha kiungo huyo ambaye ni kipenzi kikubwa cha mashabiki wa soka nchini Rwanda.

Niyonzima (34) anarejea Rayon akitokea nchini Libya alikokuwa anaitumikia Al Ta’awon iliyomaliza nafasi ya tatu kwenye ligi ya nchini humo msimu uliopita.

Rayon Sport inakuwa klabu ya nne kwa Niyonzima kuitumikia ndani ya Rwanda akianza na Etincelles, APR na AS Kigali.

Hapa Tanzania, Niyonzima alicheza kimafanikio katika klabu za Simba na Yanga na kushinda mataji matano mfululizo ya Ligi Kuu Bara, matatu akiwa Jangwani na mawili akiwa Msimbazi.

Related Posts