Rais Biden asema hatoacha kumkosoa Trump – DW – 17.07.2024

Biden ameendelea na wito wake wa kutuliza kauli za kuwatenganisha Wamarekani kutoka pande zote mbili za Democratic na Republican.

Rais huyo lakini amesema kwa kufanya hivyo haimaanishi kwamba anastahili kusita kusema ukweli kumhusu hasimu wake wa chama cha Republican, Trump.

Akizungumza katika Mkutano wa Chama cha Maendeleo ya Watu Weusi huko Marekani, NAACP, mjini Las Vegas, Biden amesema usitishwaji wa machafuko ya kisiasa nchini humo inastahili kumaanisha kumaliza umwagikaji damu wa aina yoyote ile.

“Siasa zetu zimekuwa zenye kuleta hasira mno,” alisema Biden.

Kuendelea kusema ukweli

Hilo lakini halikumzuia rais huyo wa Marekani kumshambulia Trump kwa kudai kwamba utawala wake ulikuwa mbaya kwa Wamarekani weusi.

Marekani | Mkutano Mkuu wa chama cha Republican Milwaukee | Donald Trump
Mgombea wa chama cha Republican, Donald TrumpPicha: Carolyn Kaster/AP Photo/picture alliance

“Si eti kwa kuwa tunastahili kupunguza joto la siasa zetu kwa kuwa hilo linafungamana na machafuko, haimaanishi kwamba tunastahili kuacha kusema ukweli,” alisema Biden huku wafuasi wake wakitoa kauli za kutaka kuchaguliwa kwake kwa miaka mingine minne.

Amezungumzia pia jinsi alivyolishughulikia vibaya janga la Uviko-19 na ongezeko la ukosefu wa ajira kutokana na kufungwa mapema kwa nchi.

Biden analenga kuonesha jinsi utawala wake unavyowaunga mkono wapiga kura weusi huko Marekani ambao ni kiungo muhimu kwa chama cha Democratic na yuungwaji mkono wake binafsi.

Mgombea bora wa Democratic kumshinda Trump

Rais huyo wa Marekani atashiriki katika mahojiano na televisheni ya BET na baadae kuyahutubia ya uhamasishaji wa watu Wamarekani wanaozungumza Kihispania.

Rais wa Marekani Joe Biden - Ahimizwa kujiuzulu kugombea urais
Joe Biden akishiriki mdahalo wa televisheni na Donald TrumpPicha: Justin Sullivan/Getty Images

Haya yanafanyika wakati ambapo Wademocrat wamekuwa wakijadiliana kwa kipindi cha wiki nzima kuhusiana na mzozo wa kutokuwa na imani kuhusiana na ugombea wake Biden, kutokana na jinsi alivyoboronga katika mdahalo wa televisheni dhidi ya Donald Trump mwezi uliopita.

Biden mwenye umri wa miaka 81 amekataa miito kadhaa ya kukaa kando katika kinyang’anyiro hicho cha urais, akidai kwamba yeye ndiye mgombea bora wa chama cha Democratic ambaye yuko katika nafasi nzuri zaidi ya kumshinda trump katika uchaguzi wa Novemba. 

Chanzo: APE

Related Posts