TIMU ya Goztepe S.K ya Uturuki imeonyesha nia ya kuipata saini ya nyota wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Novatus Dismas Miroshi.
Nyota huyo wa zamani wa timu za Biashara United na Azam FC, msimu uliopita alikuwa akiichezea Klabu ya SV Zulte Waregem ya Ubelgiji kwa mkopo akitokea Shakhtar Donetsk ya Ukraine na sasa miamba ya Goztepe S.K inahitaji kuipata saini yake.
DODOMA Jiji imeingilia dili la mshambuliaji wa zamani Yanga, Heritier Makambo kutoka Al Murooj SC ya Libya. Awali Mkongomani huyo aliyewahi kuzichezea DC Motema Pembe, FC Lupopo zote za DR Congo na Horoya AC ya Guinea, ilielezwa angejiunga na Tabora United japo kwa sasa mambo yamebadilika baada ya Dodoma kumtaka.
KIUNGO wa Singida Black Stars (SBS), Mnigeria Morice Chukwu amewataka viongozi kuvunja mkataba. Nyota huyo aliyejiunga Julai 16, mwaka jana akitokea Rivers United ya Nigeria amepewa barua ya kupelekwa kwa mkopo Tabora United, jambo ambalo limemkera na kuwataka viongozi kuvunja mkataba wake.
UONGOZI wa Coastal Union unaelezwa kutuma barua ya kumtaka beki wa kati wa Singida Black Stars, Laurian Omar Makame. Nyota huyo aliyejiunga na timu hiyo mwaka jana akitokea Klabu ya Black Sailor ya Zanzibar, inaelezwa anaweza akatolewa kwa mkopo ili akapate nafasi ya kucheza, japokuwa haitakuwa rahisi kwa Coastal Union kwani Yanga inamhitaji pia.