Ubabe ubabe, hawana ugenini wala nyumbani

UNAPOSIKIA neno ugenini kama nyumbani hiyo inamaanisha kwamba popote pale mechi ikipigwa ushindi unapatikana haijalishi uchache wa mashabiki wa upande wa mshindi wala wingi wake.

Katika mchezo wa ngumi, imekuwa ni kama kawaida kushuhudia mabondia wanapokuwa ugenini wanapoteza mapambano yao kwa kiwango kikubwa, ikitokea mgeni ameshinda ugenini, inakuwa stori kubwa sana.

Kupoteza mapambano kwa mabondia wanapokuwa ardhi ya ugenini kumekuwa na mambo mengi yanafichuka ikiwemo figisu wanazofanyiwa.

Mabondia wa Tanzania ni miongoni mwa waathirika wa matukio hayo ambapo mara kadhaa wamekuwa wakipoteza ugenini, lakini wapo ambao waliufanya uwanja wa ugenini kuwa kama nyumbani.

Hapa kuna mabondia wa Kitanzania ambao wamewahi kushinda mapambano yao nje ya Tanzania na kurudi nyumbani wakiwa vifua mbele, ingawa pia wameshawahi kupoteza huko ugenini.

Unapoongelea mchezo wa ngumi nchini itakuwa shida sana kama utashindwa kulitaja jina la bondia wa zamani, Rashid Matumla kutokana na makubwa aliyofanya kabla  ya kuibuka kizazi kipya.

Katika mabondia ambao wamefanikiwa kutusua katika mapambano ya kimataifa kwa mabondia wakongwe waliacha mchezo huo, Matumla yupo.

Mpaka anaacha mchezo wa ngumi mwaka 2013, Matumla alikuwa amecheza jumla ya mapambano 72, akishinda 49 kati ya hayo 34 ni kwa ‘Knockout’ yaani KO huku akipigwa mara 19 kati hizo sita zikiwa ni kwa KO pamoja na kutoka sare mara nne.

Matumla ambaye ni mtoto wa mzee Ali Matumla pamban lake la kwanza kushinda nje ya mipaka  ya Tanzania ilikuwa ni mwaka 1995 nchini Zambia baada ya kumchapa Mwenda Chama kwa Technical KnockOut ya raundi ya kwanza katika pambano la raundi kumi ambalo lilifanyika Lusaka, Zambia.

Lakini mwaka 1999 nchini Italia katika Ukumbi wa Piacenza bondia Paolo Pizzamiglio alikiona cha moto kutoka kwa Matumla kufuatia kumshushia kichapo cha TKO ya raundi ya pili katika pambano la raundi 12 ambalo Matumla alifanikiwa kushinda mkanda wa ubingwa wa dunia wa WBU kwenye uzani wa Super Welter.

Chuma hicho kutokea mitaa ya Keko jijini Dar aliendelea kusumbua wageni katika mataifa yao baada ya mwaka 2002 kumchapa Garry Murray wa  Afrika Kusini kwa TKO ya raundi ya sita katika pambano la raundi 12 ubingiwa wa kimataifa wa IBU ambalo lilifanyika kwenye hoteli ya Lord Charles Hotel, Somerset West, Afrika Kusini.

Kwa sasa ndiyo bondia namba moja nchini ambaye Jumamosi ya wikiendi hii anatarajia kupanda ulingoni kutetea mkanda wake wa ubingwa wa WBC Afrika dhidi ya Sabelo Ngebiyana katika pambano litakalopigwa kwenye Ukumbi wa Mbeya City Pub jijini Mbeya.

Majiha au Kiepe Nyani ameshacheza mapambano 50 akiwa ameshinda jumla ya mapambano 32 kati ya hayo 15 kwa KO na amepigwa mara 14 kati ya hizo tatu pekee ni kwa KO huku akitoka sare mapambano manne.

Majiha akiwa bondia pekee ambaye mwaka jana alifikia hadhi ya nyota nne  na nusu pamoja na kufika katika tano bora ya mabondia bora duniani kwenye uzani wake, amefanya maajabu makubwa kwenye mataifa ya watu.

Mwaka 2013, Majiha nchini Indonesia alifanikiwa kumchapa kwa pointi Heri Amol wa taifa hilo katika pambano la raundi sita ambalo lilipigwa kwenye Ukumbi wa Tennesi uliopo Jarkata.

Tabia ya ushindi wa nje ya Bongo kwake ikawa kawaida baada ya kufanya kitu kibaya, Gabriel Ochieng wa Kenya katika pambano la kuwania mkanda wa ubingwa wa WBA Pan Afrika  lililopigwa kwenye Hoteli ya Crowne Plaza, Nairobi kwa Majiha kushinda ubingwa huo, pambano lilipigwa mwaka 2017.

Mwaka 2018, Majiha alifanikiwa kutetea mkanda wake a ubingwa wa WBA Pan Afrika nchini  Afrika Kusini baada ya kumpiga kwa pointi Rofhiwa Nemushungwa katika pambano la raundi 12 ambalo lilipigwa kwenye Ukumbi wa Carnival City Casino, Brakpan, Afrika Kusini.

Bingwa huyo wa WBC Afrika, mwaka 2021 alihamishia balaa lake la kutoa vichapo katika ardhi ya Mfalme Charles III wa Uingereza kwa kumpiga Harvey Horn kwa TKO ya raundi ya nne katika pambano la raundi kumi ambalo lilifanyika kwenye Ukumbi wa York Hall, Bethnal Green, Uingereza.

Ni mdogo wa bingwa wa zamani wa ngumi za kulipwa nchini Francis Cheka ambaye amekuwa na rekodi kubwa kimataifa zaidi ya kaka yake lakini hatajwi.

Cheka ambaye amecheza jumla ya mapambano 57 akiwa amefanikiwa kushinda 29 kati ya hayo mapambano saba ameshinda kwa KO na amepigwa katika mapambano 20,  nane yakiwa ni KO huku akitoka sare mapambano nane.

Jina lake limebaki katika vitabu vya kumbukumbu nchini Thailand baada ya kushinda ubingwa wa WBO Asia Pasific kwa kumchapa kwa TKO, Aphinan Rengron katika pambano ambalo lilipigwa kwenye Kituo cha Maduka ya Westgate, Bang Yai, Thailand.

Mwaka 2017 katika viwanja vya Carnivore, Nairobi nchini Kenya, Cheka alimtandika Mkenya,David Rajuili kwa TKO ya raundi ya nane katika pambano la raundi kumi.

Lakini Disemba mwaka 2017, alirejea tena Kenya katika Viwanja ya Carnivore jijini Nairobi ambapo safari hii alimteketeza kwa ushindi wa pointi Kenneth Kidega katika pambano la raundi nane.

Utawala wa Cheka nchini Kenya ulikuwa mkubwa kabla ya kutoa kipigo cha mwisho mwaka 2018 kwa Geoffrey Nyamu ambapo alimchapa kwa pointi katika pambano la raundi sita ambalo lilipigwa kwenye Viwanja vya Kibera Kamukunji, Nairobi,Kenya.

Licha kuonekana ameteketea kiuwezo ndani ya ulingo lakini Dullah Mbabe ni mmoja kati ya mabondia wanaostahili heshima kubwa kutokana na makubwa aliowahi kufanya nje ya Bongo.

Bondia huyo mwenye rekodi ya kucheza mapambano 50 akiwa amefanikiwa kushinda 34 kati ya hayo 29 ni kwa KO na amepigwa mara 14 kati ya hizo mara tatu pekee ni KO na ametoka sare moja.

Mwaka 2016, Mrusi Andrey Kalyuzhnyy nchini China kwenye Ukumbi wa michezo wa Shanghai Oriental alikiona cha moto kutoka kwa Dullah Mbabe baada ya kumchapa kwa TKO ya raundi ya tatu katika pambano la raundi sita.

Mwaka 2019,  Dullah Mbabe alifanikiwa kushinda mkanda wa ubingwa wa WBO Asia Pasific kwa kumchapa Mchina,    Zulipikaer Maimaitiali kwa TKO ya raundi ya tatu katika pambano la raundi kumi.

Kijana kutoka Bagamoyo mkoani Pwani, Maono Ally ndiye Mtanzania na bondia wa kwanza nchini kushinda mkanda wa ubingwa wa Baraza la Ngumi Duniani, WBC.

Maono, mwenye rekodi ya kucheza mapambano 25 ambapo amefanikiwa kushinda 15 kati ya hayo 11 ni kwa KO na amepigwa tisa kati ya hayo matano ni kwa KO na ametoka sare moja.

Mwaka 2018, Luka Pupek kutoka Crotia alikiona cha moto kutoka kwa Maono baada ya kukubali kuchapika kwa TKO ya raundi ya pili katika pambano la raundi kumi ambalo Mtanzania huyo akashinda mkanda wa ubingwa wa WBC Youth.

Lakini mwaka 2022 alifanikiwa kumchapa kwa TKO ya raundi pili katika pambano la raundi sita, Yaser Yuksel wa Ujerumani, pambano ambalo lilifanyika Dubai.

Sifa yake kubwa kwa sasa maneno na kejeli kwa baadhi ya wapinzani wake nchini lakini Mwakinyo ni mmoja kati ya mabondia wenye heshima ya ndani ya ulingo nje ya mipaka ya Bongo.

Mwakinyo mwenye rekodi ya kucheza mapambano 26 akiwa amefanikiwa kushinda 23 kati ya hayo 16 ni kwa KO, amepigwa mara tatu na mbili ni KO.

Mwaka 2017, Mtanzania huyo alianikiwa kushinda ubingwa wa WBA  Pan Afrika kwa kumchapa kwa pointi Anthony Jarman katika pambano ambalo lilipigwa Gaborone, Botswana.

Lakini mwaka 2018, Mwakinyo akaweka rekodi ya kumchapa Sam Eggington wa Uingereza kwa TKO ya raundi ya pili katika pambano la raundi kumi lilifanyika Birmingham, Uingereza kabla 2019,  kumchapa Sergio Gonzalez wa Argentina  katika pambano lililofanyika Kenya.

Bingwa wa zamani wa ABU, Tony Rashid akiwa na rekodi ya kucheza mapambano 22 akifanikiwa kushinda 16 kati ya hayo 11 ni kwa KO huku akiwa amepoteza manne kati ya hayo mawili ni kwa KO na sare mbili.

Mwaka 2019, Tony aweka rekodi ya kushinda mkanda wa ubingwa  wa ABU kwa kumchapa kwa TKO ya raundi kumi katika pambano la raundi 12, Siboniso Gonya, pambano lilipigwa Afrika Kusini.

Rekodi ya mapambano 38 akiwa ameshinda 32 kati ya hayo 15 ni kwa KO huku akiwa amepigwa mara sita kati hizo tatu ni kwa KO.

Mwaka 2014, Class alifanikiwa kushinda kwa TKO ya raundi tisa katika pambano la raundi kumi ambapo alifanikiwa kushinda ubingwa wa WPBF dhidi ya Mwansa Kabinga nchini Zambia.

Lakini 2016, Mtanzania huyo alishinda tena kwa pointi dhidi ya Zapir Rasulov wa Urusi katika pambano ambalo lilipigwa Panama kabla ya mwaka 2017 kushinda ubingwa wa GBCW dhidi Jose Forero wa Panama katika pambano ambalo lilipigwa Ujerumani.

Related Posts