Vivutio vya utalii Rungwe huvutia watalii 5,000 wa ndani kila mwaka

Mbeya. Licha ya watalii wa ndani 5,000 kutembelea vivutio vya utalii Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya karibu kila mwaka, bado mikakati kadhaa inaendelea kuwekwa kwa lengo la kuendeleza kampeni ya kuvitangaza ili kuvutia watalii zaidi kutoka mataifa mbalimbali.

Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kutumia fursa za nyimbo za ngoma za asili, dini, maonyesho ya sikukuu ya wakulima Nanenane na fursa za uwekezaji katika miundombinu mbalimbali.

Inaelezwa kuwa Wilaya ya Rungwe ina  vivutio vya utalii zaidi 25 huku watalii wa ndani kupitia makundi ya kijamii, wakipenda kuvitembelea  likiwamo Ziwa Ngosi, Daraja la Mungu, Kisiba, Mlima Rungwe na majengo ya mkoloni wa Kijerumani.

Akizungumza na Mwananchi Digital Leo Jumatano Julai 17, 2024, Ofisa Utalii  wa Halmashauri ya Rungwe, Numwagile Bugali amesema bado mwamko ni mdogo.

Hivyo, amesema tayari wameweka mikakati ya kuhakikisha vinatangazwa zaidi ili kuvutia  wageni kutoka mataifa mbalimbali kuja nchini.

Bugali amesema asilimia kubwa ya watalii wanaotembelea vivutio hivyo kwa sasa ni wa ndani.

“Kuna vivutio vingi sana vya utalii eneo hili la Rungwe, tunaendelea kuviibua na kuvitangaza sambamba na kutaka wawekezaji kutumia fursa hiyo kwa sababu Serikali tayari imetenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji katika sekta ya utalii,” amesema Bugali.

Mwananchi imezungumza pia na Mkurugenzi wa Kituo cha sanaa na utamaduni cha Kimondo, Bahati Longopa ameshauri Serikali kuendelea kuvitangaza vivutio hivyo kwa sababu wakazi wengi wa ukanda huo hawana elimu ya utalii.

“Changamoto elimu bado ni ndogo sana  asilimia kubwa ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini  wanaenda fukwe ya Ziwa Nyasa eneo la Matema kujipumzisha na siku za mwisho wa wiki, ndilo eneo pekee wanalitambua,” amesema Longopa.

Naye Ofisa michezo na utamaduni Wilaya ya Rungwe, Enzi Seme amesema ili kukuza utalii kwa sasa, wanashirikiana na wadau  kuandaa matamasha ya michezo  yanayosaidia kufikisha ujumbe unaozungumzia umuhimu wa kuvitangaza  vivutio vya utaliii.

Mkazi wa Kiwira Wilaya ya Rungwe, Theresia Adamson ameshauri Serikali kuboresha miundombinu ya barabara ziendazo kwenye vivutio hivyo kusudi watu wahamasike.

“Lakini nao wawekezaji wa kizawa wavutiwe kuwekeza huko ili kuchochea uchumi na kuongeza ajira kwa vijana waliokosa fursa za kuajiriwa na kujiajiri,” amesema.

Related Posts