Mashambulizi hayo yametokana na video yake iliyosambaa akizungumza kwenye tukio moja mjini Bukoba, akimhakikishia ushindi Mbunge wa jimbo hilo, Steven Byabato, kuwa matokeo ya kura siyo lazima yawe ya kwenye sanduku la kura, bali inategemea nani anahesabu kura na kutangaza matokeo.
Ingawa Nape kupitia video nyingine iliyosambaa baadaye aliomba radhi kutokana na kauli hiyo, akidai ilikuwa ni utani, kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari imezua mijadala mipana, wachangiaji wakiilaani na kuitaja kuwa imechafua hali ya hewa.
Kauli hiyo pia imezua taharuki ndani ya Serikali na CCM hadi Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa chama hicho tawala, Amos Makalla akijitokeza hadharani haraka kujitenga nayo, akisema si ya chama.
Alichotamka Nape kinarejesha kumbukumbu ya kauli ya awali aliyoitoa Juni 2015, miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu, wakati huo akiwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, kuwa chama hicho kingehakikisha kinarudi Ikulu hata kama ni kwa bao la mkono.
Neno ‘bao la mkono’ hutumiwa kama goli lililofugwa kwa kuupiga mpira kwa mkono kinyume cha taratibu za mchezo wa soka, lakini hukubaliwa kuwa goli halali kwa kuwa mwamuzi anakuwa hajaona au amepotezea kitendo kilichofanywa na mfungaji.
Kufuatia kauli hizo, wasomi na wachambuzi wa siasa, wanasema kauli ya Nape si tu imetonesha kidonda cha Uchaguzi Mkuu wa 2015 na 2020, na uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa 2019, bali ni kinyume cha ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kufanya uchaguzi huru wa na haki.
Kwa nyakati tofauti, Rais Samia na Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Abdulrahman Kinana wametoa kauli za kuwahakikishia Watanzania kuwa uchaguzi ujao utakuwa huru na wa haki.
Kwa mujibu wa ofisa mmoja wa Serikali kutoka taasisi nyeti, kauli ya Nape inavuruga dhamira njema ya Rais Samia kupitia falsafa yake ya R4, yenye lengo la kutibu majeraha na kurejesha umoja na mshikamano, baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Dk Rugemeleza Nshala alipozungumza na Mwananchi amesema analaani kauli ya Nape juu ya wizi wa kura.
“Kauli hiyo ni kama ile aliyoitoa 2015 juu ya goli la mkono. Ni uthibitisho wa kuwapo njama za kupindua uchaguzi nchini. Ni jukumu la kila mtu anayeitakia mema nchi yetu kupinga na kulaani kauli hiyo. Amepoteza sifa ya kuwa kiongozi,” almeeleza Dk Nshala.
“Tume ya Taifa ya Uchaguzi kama ina chembe ya uhuru na kujali demokrasia lazima iwahakikishie Watanzania inaheshimu maamuzi yao. Ukimya wake itakuwa ni ishara kwamba hatutakuwa na uchaguzi huru na wa haki 2024 na mwakani,” amesema.
Akiwa katika mikutano ya hadhara mkoani Arusha Julai 16, 2024, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amesema anamshangaa “Nape kujivunia uharamu na kutangaza ataiba kura kwenye uchaguzi ujao”, jambo ambalo ni hatari kwa nchi.
Akizungumza mjini Bukoba, Nape aliwataka wagombea wengine katika uchaguzi mkuu 2025 wamwachie Byabato aendee na ubunge, akisema atamsaidia ashinde kwa kuwa yeye ni mjanja wa masuala ya uchaguzi.
“Unajua ninyi sikilizeni. Matokeo ya kura siyo lazima yawe yale ya kwenye box (sanduku la kura), inategemea nani anahesabu na kutangaza na kuna mbinu nyingi. Kuna halali, kuna nusu halali na kuna haramu.
“Na zote zinaweza kutumika ilimradi tu ukishamaliza unamwambia Mwenyezi Mungu nisamehe. Kwa hiyo wanaotaka kushindana naye (Byabato) wajipange.
“Mmenielewa? Wafanye nini? Wajipange,” amesema Nape kupitia video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Mara baada ya kauli hiyo kusambaa, Katibu wa Itikadi na Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla alijitokeza na kujitenga nayo.
“Chama cha Mapinduzi kimejipanga kushinda kwa haki. CCM haihitaji mbeleko. CCM itashinda kwa haki kwa sababu tunayo rekodi nzuri ya kuwaletea wananchi maendeleo. Kauli hiyo ipokewe kuwa si ya Chama cha Mapinduzi,” amesema Makalla.
“Kauli ya kupokewa ni hii. CCM inaheshimu demokrasia, inaamini kwamba vyama vyote vitashindana na Chama cha Mapinduzi na CCM kitashinda kwa haki. CCM kitaheshimu matokeo yoyote, uamuzi wowote wa wananchi kupitia sanduku la kura na kwamba aliyeshinda kwa haki ndiye atakayetangazwa,” amesema.
Baada ya mjadala huo kuwa moto, Nape kupitia ukurasa wake wa X (zamani twitter) aliandika ufafanuzi ambao hata hivyo, haukutuliza mjadala.
“Msingi wa mjadala ulikuwa utani wa hoja ya zamani ya ‘goli la mkono’ uliorushwa wakati naongea, ndiyo maana kuna kicheko kabla. Haikuwa serious version. Mimi ni muumini wa uchaguzi huru na haki. Vizuri tuendelee kushindana kwa hoja.”
Huku ukosoaji ukiendelea, Nape alirekodi video na kuisambaza mitandaoni akisisitiza ulikuwa utani wenye historia ndefu ya miaka tisa, alipohusishwa na kauli ya goli la mkono mwaka 2015 na kwamba utani huo umeendelea kwa miaka yote.
“Niseme kama kiongozi, mtu mzima nadhani nawajibika kuwapa pole wale ambao wamesumbuliwa na wameteseka na wamepata tabu na huu mjadala, kuwapa pole na kuomba radhi na nasisitiza kwamba ulikuwa ni utani,” amesema Nape.
Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alidai kauli ya Nape ndiyo msimamo wa CCM, japo wamekanusha.
“Kauli ya Nape inaashiria kile kilichopangwa ndani ya Serikali na chama, hivyo kwanza Rais Samia anapaswa kutengua uteuzi wa Waziri Nape,” amesema.
Kwa mujibu wa Mnyika, kauli hiyo inaonyesha huenda ni sababu ya Rais Samia kutoridhia mabadiliko ya kikatiba na kisheria kuwezesha uchaguzi kuwa huru na haki na hata katika sheria mpya iliyotungwa wamelazimisha tume iliyopo iendelee kufanya kazi.
Mnyika ameitafsiri kauli hiyo ni sababu ya Serikali kukataa uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji kusimamiwa na Tume Huru ya Uchaguzi, akisisitiza wananchi hawatakuwa tayari kuona uchaguzi unaingiliwa ilivyotokea mwaka 2020.
Aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba amesema kilichotamkwa na kiongozi huyo ni dharau kwa wananchi.
“Huyu anaeleza kuwa kura zetu hazina maana, ameshasema na siyo mara moja, najua yamekanushwa lakini haitoshi, kama Rais Samia hawezi kuchukua hatua hakuna sababu ya kuendelea na uchaguzi, huku ni kupoteza muda,” amesema.
Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Bob Chacha Wangwe amesema kauli hiyo si tu inaonyesha ni kwa kiasi gani nchi inaongozwa na viongozi wengi wasiokuwa na maadili, bali wasio na hofu ya Mungu.
“Kauli ambayo inadhihirisha ni kiasi gani Watanzania ni wavumilivu, kauli za namna hiyo zingetosha kuwafanya kuachia ngazi kwa kujiuzulu au kwa mamlaka ya uteuzi kutengua nafasi zao,” amesema.
Wangwe amesema Nape alipaswa kujiuzulu, kwani kauli za namna hiyo ni hatari hata kwa usalama wa nchi. Amesema unyang’anyi na wizi ni dhambi na lazima yeyote anayehamasisha dhambi awajibike bila kujali nafasi yake au sehemu anayohamasishia.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie amesema “hiki ni kiburi cha madaraka, wameshaona wapo madarakani kwani watafanywa nini, wengi wanaotoa kauli hizi wanakuwa wametoa siri, yaani ‘vifua havigandishi’ na huwa wanapata nafasi nzuri za uteuzi.”
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Buberwa Kaiza amesema kauli ya Nape na viongozi wengine ndiyo uhalisia uliopo, japo CCM imekanusha.
“Hata wale wengine ambao hawakutamka, hivyo ndivyo wanavyojua na ndiyo mpango wao. Nilitamani kwa kauli hii ambayo inakiuka sheria hatua kali zingechukuliwa,” amesema.
Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma wa ACT-Wazalendo, Shangwe Ayo amesema wanajua Nape alidhamiria na hata msamaha aliowaomba Watanzania ni kuwahadaa.
“Tunashangaa hata Rais Samia ambaye amempatia madaraka ya uwaziri, hajatoka kukemea kitendo hicho, ina maana anaunga mkono. Tunamtumia ujumbe Nape ACT tunaenda kuwaandaa Watanzania kupiga kura na kuzilinda kura zao vituoni,” amesema.
Amesema Nape anapaswa kujua Tanzania ni nchi inayozingatia misingi ya kidemokrasia.
Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano Chama cha Wananchi (CUF), Mohamed Ngulangwa amesema kauli ya Nape ni mbaya, lakini isiyoshangaza.
“Aliwahi kutoa kauli kama hii mwaka 2015, baada ya hayati Rais John Magufuli kuingia madarakani, alipewa uwaziri na alipambana na demokrasia nchini kwa kuzuia Bunge kurushwa moja kwa moja na kusimamia sheria kali kwa vyombo vya habari hivyo,” amesema.
Ngulangwa amesema kauli ya Nape inashangaza kwa sababu wakati ambao Rais Samia anatafuta namna ya kuileta nchi pamoja, anatumia watu wasio sahihi.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.