KAMATI ya Olimpiki Tanzania (TOC) imesema msafara wa Tanzania kwenye michezo ya Olimpiki msimu huu utaondoka nchini kwa mafungu.
Kundi la kwanza litaondoka Julai 22 likiwa na mkuu wa msafara, Henry Tandau. Imesema, kundi la pili litaondoka Juali 23 na kundi la mwisho ni la wanariadha watakaoondoka Agosti 7 tayari kwa michezo hiyo itakayofunguliwa Julai 27 hadi Agosti 11.
Akifafanua kilichochangia timu hiyo yenye wanariadha wanne, waogeleaji wawili na mcheza judo mmoja kuondoka kwa mafungu, Tandau amesema ni kutokana na upatikanaji wa tiketi na utaratibu wa waandaaji nchini Ufaransa inapofanyika.
“Mkuu wa msafara anatakiwa kuwahi mapema ili kuweka mambo sawa kwa timu yake itakapowasili kwenye kijiji cha michezo, pia upatikanaji wa tiketi kwa wachezaji, wetu umechangia timu iondoke kwa mafungu,” amesema.
Aliwataja wachezaji watakaoiwakilisha nchi kuwa ni waogeleaji Collins Saliboko na Sophia Latiff na mcheza judo, Andrew Mlugu ambao wamepata nafasi ya upendeleo
Wengine ni wanariadha wa marathoni, Jackline Sakilu, Magdalena Shauri, Alphonce Simbu na Gabriel Geay waliofikia viwango vya kushiriki Olimpiki msimu huu.
Tandau amesema msafara wa Tanzania pia utakuwa na makocha watatu, daktari wa timu na mwandishi.
“Pia waziri wa michezo na msaidizi wake na rais wa Kamati ya Olimpiki (Gulam Rashid) na Katibu Mkuu (Filbert Bayi) wao watakwenda kwa ajili ya vikao.
Amesema, timu ya Tanzania itaagwa Julai 19 kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Awali, harakati za kufuzu zilishirikisha pia timu ya soka la wanawake, ngumi na brake dance ambazo zilishindwa kufikia viwango.
Tofauti na ilivyozoeleka, msimu huu mbio ya marathoni inatarajiwa kukimbiwa usiku, Tanzania ikiwakilishwa na Simbu, Geay, Sakilu na Shauri ambao wanatazamwa kuvunja rekodi ya 1980 ambayo nchi ilishinda medali mbili za fedha kwenye michezo hiyo kwa mara ya kwanza, rekodi ambayo haijawahi kuvunjwa.