Washika usukani 18 mzigoni mbio za magari

VUMBI jekundu eneo la Pongwe, Kisimatui, Mkanyageni na Mlamleni mkoani Tanga litatimka Jumamosi wakati madereva 18 watakapokuwa kibaruani kuwania ubingwa wa mbio magari za ufunguzi wa msimu zinazoitwa Advent Rally of Tanga

Hayo ni mashindano ya kwanza ya ubingwa wa taifa kwa mbio za magari ambayo yatashirikisha madereva kutoka ndani na nje ya nchi, kwa mujibu wa Hussein Moor wa  klabu ya Mount Usambara, ambao ndiyo waandaaji wa mbio hizo.

“Kila kitu kiko  sawa na madereva wameanza kuwasili mjini Tanga tangu Jumatano (jana) kwa ajili ya kukamilisha taratibu za mashindano,” alisema Moor.

Kwa mujibu ratiba ya matukio, Jumamosi asubuhi,  madereva na wasoma ramani wataanza kwa zoezi la kukagua barabara (raking) zitakazotumika ili kuhakiki maeneo korofi kwa ajili ya usalama.

“Baada ya zoezi hili jioni tutakuwa na ukaguzi wa magari (scrutineering)  kabla ya kuyapasisha kwa mashindano baada ya kukidhi vigezo vyote vya usalama,” alifafanua Moor.

“Tunategemea kuona ushindani mkali katika mbio hizi kwani kila dereva atakuwa akiwania alama nzuri zitakazompa ubingwa wa taifa mwishoni mwa msimu.”

Baada ya hatua zote kukamilika, mashindano yataanza Jumapili, Julai 21 na magari yatatoka Tanga mjini kuelekea Pongwe ambako sehemu kubwa ya mbio zitafanyika.

Umbali wa njia kuu ya mashindano ni kilomita 155  na magari yatachuana katika maeneo yenye vivutio vya utalii.

Hadi kufikia jana ni dereva mwongozaji David Sihoka kutoka Zambia ndiye  wa nje aliyethibitishwa kushiriki akimuongoza Gurpal Sandhu wa Arusha ndani ya Mitsubishi Evo 10.

Madereva gwiji kutoka Tanzania ambao  wamethibitisha kushiriki ni Randeep Birdi kutoka Dar es Salaam na ndugu yake Manvir Birdi ambao wataendesha gari aina ya Mitsubishi Evo 9.

Related Posts