WATUMISHI WA AFYA ZINGATIENI MAADILI YA KAZI KAZINI.

Naibu Waiziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Elimu Mhe. Dkt. Festo Dugange (Mb) amewataka Watumishi wa Sekta ya Afya kote Nchini kuhakikisha wanazingatia utoaji wa huduma kwa kuzingatia Maadili, Lugha nzuri na Uwajibikaji kutokana na viapo vyao vya ya kazi pindi wawapo kazini.

Mhe. Dkt. Dugange ametoa maelekezo hayo leo Julai 16,2024 katika hafla fupi ya Makabidhianao Majengo ya utoaji Huduma ya Uzazi na Mtoto katika kituo cha Afya Haneti kwa ufadhili wa Shirika la KOICA kupitia Shirika la UNICEF Wilayani Chamwino mkoani Dodoma

“Pamoja na kazi nzuri ambazo watumishi wa Afya wamekuwa wakifanya lakini kuna baadhi ya watumishi wa sekta ya Afya wamekuwa wakitoa huduma bila kuzingztia maadili, lugha nzuri na uwajibikaji kulingana na viapo vyao, hivyo nawakumbusha watumishi wote wa sekta ya afya nchini kuzingatia maadili katika utoaji wa Huduma.”

Aidha Dkt. Dugange amesema Tanzania imeendelea kupiga hatua katika kuongeza miundombinu ya upatikanaji wa huduma za Afya hususani huduma za dharura za upasuaji kwa akina mama wajawazito kutoka vituo 115 mwaka 2017 hadi kufikia vituo 503 Juni ,2023. Hatua hizi zimesaidia sana katika kuongeza kasi ya kupunguza vifo vinavyotokana na Uzazi na vifo vya watoto wachanga.

Amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la akinamama wajawazito wanaohudhuria kliniki mara nne na zaidi toka 51% (TDHS 2015/16) mpaka 86% kwa takwimu za mwaka 2022. Vilevile,kiwango cha wajawazito wanaojifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kimeongezeka kutoka 63% (TDHS 2015/16) mpaka 80% (TDHS-2021-2022).

Pia Dkt. Dugange ametoa maelekezo watendaji wote wa Sekta ya Afya na viongozi wa mamlaka za serikali za mitaa kuendelea kutekeleza Sera ya Afya ya matibabu bila malipo kwa wakinamama Wajawazito na Watoto chini ya Miaka Mitano ni lazima itekelezwe kwani Serikali imekuwa ikilipia huduma hizo.

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa KOICA Ndugu. Manshik Shin- amesema serikali ya Korea itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Nyanja mbalimbali kama vile Uchumi, Kijamii na Kisiasa ikijumuisha ujenzi wa Miundombinu ya Afya, Mawasiliano na Elimu ili kuwezesha utoaji wa Huduma mbalimbali kwa Wananchi.



Related Posts