Dar es Salaam. Hofu imezidi kuwakumba wazazi na shule jijini Dar es Salaam kutokana na matukio ya watoto kupotea.
Wasiwasi umechangiwa na tukio la hivi karibuni lililotokea Mbagala wilayani Temeke, Dar es Salaam, ambako Yusra Mussa, mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Mbagala Kuu, aliuawa ikidaiwa baadhi ya viungo vya mwili wake, ikiwamo figo iliondolewa.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ilisema tangu Machi Jeshi hilo limepokea taarifa nne kutoka kwa wazazi wa Mbagala na Temeke na kati ya matukio hayo matatu yalisababisha vifo vya watoto waliotendewa ukatili.
Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Jumanne Muliro alikana watoto hao kuondolewa viungo
Ingawa hakuna takwimu sahihi za watoto kupotea katika jiji hilo, lakini matukio haya yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara kwenye vyombo vya habari.
Mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam, Faudhia Rashid (43) alisema, “Kama mzazi, nina wasiwasi mkubwa kutokana na ongezeko la matukio ya watoto kupotea. Tunahitaji hatua bora za usalama na mwamko zaidi ili kuwalinda watoto wetu.”
Mzazi mwingine, Fausta Bernard (32) aliyewahi kupoteza mtoto wakati wa sherehe za mwaka mpya wa 2024 alisema: “Matukio ya hivi karibuni ya watoto kupotea yamenitia hofu na wasiwasi, nahakikisha ninamsindikiza mtoto shuleni, na nakwenda kumchukua. Tunahitaji kushirikiana kwa karibu na shule na mamlaka ili kuhakikisha usalama wa watoto wetu.”
Nehemia Sayuni mkazi wa Mabibo amesema, “Tunahitaji tahadhari kubwa kwa jamii na polisi kuitikia kwa haraka matukio haya.”
Baadhi ya shule zimeanza kutoa tahadhali kwa wazazi na walezi kuhusu suala hilo.
Taarifa iliyosainiwa na mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi ya Kiislamu Kongowe, Said Hassan inawataka wazazi kuhakikisha watoto wao wanafikishwa shuleni na kukabidhiwa kwa mlinzi kati ya saa 12.30 asubuhi na saa 1.00 asubuhi.
Pia inamtaka mzazi kumjulisha mwalimu wa darasa au mlinzi wa shule kuhusu mabadiliko ya mtu kwenda kumchukua mtoto shule na muda wa mwisho kumchukua ni saa 11:30 jioni.
Kwa wanaotumia usafiri wa shule, taarifa inawataka wazazi kuwa kwenye vituo vya mabasi ili kuwakabidhi na kuwapokea watoto wao kwa wakati.
Wanaochukua watoto lazima wajiandikishe getini shuleni kuepuka kufahamiana kusikokuwa kwa lazima.
“Wazazi na walezi tushirikiane kuendelea kuwaelimisha watoto kuhusu mazingira hatarishi waweze kuelewa na kuwa waangalifu zaidi. Hii ni pamoja na kuepuka mazungumzo ya muda mrefu na watu wasiowafahamu, bali iwe salamu tu, hasa kwa wanafunzi wenye uwezo wa kufika shuleni wenyewe,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi akizungumza na Mwananchi amesema kila mtu ana haki ya kulindwa, hasa watoto kwa sababu hawawezi kujitetea.
“Kutoweka kwa watoto kunaonyesha bado kuna mapungufu katika kuwalinda ndiyo maana matukio haya yanatokea na kusababisha hofu miongoni mwa jamii,” amesema.
Amependekeza kila mmoja kuwajibika katika majukumu yake, na Jeshi la Polisi lichukue hatua mara moja linapofahamishwa kuhusu mtoto aliyepotea kwani ni tukio la dharura, siyo lililopangwa.
Mratibu wa Umoja wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa amesema kuna haja kwa Polisi kuongeza umakini katika kuwatafuta watoto waliopotea.
“Ikiwa mtoto hayuko katika eneo linalotarajiwa, polisi wanapaswa kuanza uchunguzi mara moja baada ya kupokea taarifa. Hatua hii ya haraka ni muhimu katika kuongeza nafasi ya kuwapata watoto waliopotea,” amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Anna Henga amesema wazazi, walezi, walimu na mtu yeyote anayefanya kazi moja kwa moja na watoto anatakiwa kuonyesha juhudi za ziada kuhakikisha watoto wanacheza na kujumuika katika maeneo wanayoweza kuonekana kwa urahisi.