MASHABIKI wa Yanga hadi sasa bado hawaelewi kinachoendelea klabuni kwao, baada ya tangu juzi usiku kuenea kwa taarifa kwamba uongozi wa klabu hiyo hautambuliwi kisheria kutokana na hukumu ya kesi iliyofunguliwa na baadhi ya wanachama kupinga katiba iliyowaingiza madarakani.
Hata hivyo, sakata hilo la wanachama hao kuipinga katiba ya mwaka 2010 inayolikataa Baraza la Wadhamini wa klabu hiyo, limechukua sura mpya baada ya uongozi wa Yanga jana kuzungumza jijini Dar es Salaam na kumtoa msimamo, huku mmoja ya wanachama waliofungua kesi hiyo akitoa ufafanuzi wa suala zima lilivyo, akisisitiza hana tatizo na uongozi uliopo, isipokuwa analia na katiba ya klabu hiyo.
Awali, juzi usiku ilielezwa Yanga ilikuwa imepokea hukumu ya kutotambulika kwa Baraza la Wadhamini la klabu hiyo kufuatia hukumu iliyotolewa Agosti 2, 2023.
Hukumu hiyo ambayo Mwanaspoti limeipata nakala yake, kufuatia kesi ya msingi iliyofunguliwa Agosti 4, 2022 na walalamikaji Juma Ally na Geoffrey Mwaipopo ikitaka kutotambulika kwa Baraza la wadhamini la Yanga lililoweka madarakani kwa katiba ya 2010 iliyorekebishwa mwaka 2011 kukosa sifa kisheria.
Aidha, walalamikaji pia walitaka miamala yote ya fedha iliyoidhinishwa na baraza hilo, kutotambulika na kuwa ni batili.
Hukumu hiyo, imeitaka bodi iliyokuwa madarakani kwa katiba ya mwaka 1968 iliyofanyiwa mabadiliko mwaka 2011 kurudi madarakani kuongoza klabu ya Yanga.
Inaelezwa walalamikaji walirudi mahakamani kukazia hukumu hiyo kwa kuiondoa madarakani bodi hiyo wadhamini ndipo uongozi wa sasa wa Yanga ukapenyezewa taarifa.
Maamuzi hayo yanaliweka matatani baraza hilo la Wadhamini la Yanga linaongozwa na Mwenyekiti Kapteni Mstaafu George Mkuchika na wajumbe ambao ni; Mama Fatma Karume, Dk Mwigulu Nchemba, Tarimba Abbas na Antony Mavunde.
Hata hivyo, uongozi wa Yanga jana katika mkutano na wanahabari ulisema umeomba kuongezewa muda wa kufanya mapitio ya kesi kwa Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu inayouondoa uongozi uliopo madarakani chini ya Injinia Hersi Saidi.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Sheria wa klabu hiyo, Simon Patrick wakati akitoa ufafanuzi wa hukumu ya kesi iliyotolewa Agosti, mwaka jana na Mahakama hiyo.
Patrick alisema mbali ya kuchukua hatua hiyo, klabu pia itapeleka maombi ya kufanya marejeo ya kesi hiyo ambayo ilifunguliwa na Juma Ally na Geofrey Mwaipopo dhidi ya Wajumbe wa Baraza la Wadhamini wa klabu hiyo.
Alisema kuwa wameamua kufanya hivyo kwa sababu suala hilo ni la kisheria na hasa ukizingatia kuwa muda wa kufanya marejeo na kukata rufaa umekwisha bila wao kuwa na taarifa kutokana na ukweli kuwa uongozi haukuwa na wito wa mahakama.
Patrick alisema, wao walijua kuwepo wa kesi hiyo Juni 16 mwaka huu muda ambao usingeweza kuchukua hatua yoyote kutokana na sababu kutopata taarifa.
“Mbali ya mambo hayo mawili, uongozi pia utawasilisha rasmi maombi ya kuzuia utekelezaji wa hukumu ambayo inawaondoa madarakani, huku ikitangaza mpango wa kuchukua hatua ya kisheria ikiwa pamoja na kufungua kesi ya jinai dhidi ya Abeid Mohamed Abeid wanayetuhumu kufanya kosa la kugushi saini za mama Fatuma Karume na Jabir Katundu.
“Pia tutafanya uchunguzi wa kina kujua wanachama waliokuwa ‘nyuma’ ya walalamikaji na wakibainika, watapelekwa katika mkutano mkuu wa wanachama kwa hatua zaidi,” alisema Patrick.
Akifafanua zaidi, alisema wameamua kufanya mambo hayo matano kutokana na hujuma zilizopo dhidi ya klabu yao kwani pia wamegundua kuwa Juma Ally, Geofrey Mwaipopo na Abeid Mohamed Abeid sio wanachama halali wa klabu hiyo.
“Baada ya kupata hukumu, tuliomba Makahama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu kufanya upekuzi wa kesi na kugundua mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na ujanja ujanja ambao uliokuwa unatumika.
“Kwanza, wito wa kuitwa mahakamani ulikuwa unapokelewa na Abeid Mohamed Abeid ambaye alijtambulisha kuwa anawawakilisha wadhamini wengine na klabu kwa ujumla. Abeid alikuwa anakubali kila hoja iliyokuwa inatolewa mahakamani dhidi ya uongozi wa klabu,” alisema Patrick.
Kesi hiyo ilifunguliwa Agosti 4, 2022 ambapo walalamikaji walipinga kutambuliwa kwa Bodi ya Wadhamini ya Yanga, ambayo ilianzishwa chini ya katiba ya mwaka 2010, wakitaja upungufu wa kisheria.
Katika hukumu yake, mahakama iliamuru Bodi ya Wadhamini ya Yanga chini ya katiba ya mwaka 1968 iliyorekebishwa mwaka 2011, irejee kwenye majukumu ya kusimamia na kuendesha shughuli za klabu hiyo.
Zaidi, mahakama pia iliamua kuwa Bodi ya Wadhamini chini ya katiba ya mwaka 1968 iliyorekebishwa mwaka 2011 inapaswa kuandaa, kuitisha, na kuwezesha mkutano wa wanachama wa klabu kwa madhumuni ya kuchagua wanachama wapya wa Bodi ya Wadhamini.
Kwa sasa, Bodi ya Wadhamini wa Yanga ipo chini ya Mwenyekiti George Mkuchika na wajumbe Mama Fatuma Karume, Mwigulu Nchemba, Tarimba Abbas na Antony Mavunde.
Mmoja wa mlalamikaji Juma Ally Magoma akidai hana shida na uongozi uliopo madarakani na kwamba tatizo lake ni katiba ya klabu hiyo.
Akizungumza jana, Magoma alisema uongozi uliopo madarakani chini ya Rais Injinia Hersi Said hana tatizo nao, lakini namna katiba ya klabu inavyosimamiwa ndivyo inavyompa shida.
Magoma alisema tatizo la Katiba ya Yanga ilianzia katika mabadiliko ya katiba hiyo yaliyofanyika Juni 27, 2021 kwenye Ukumbi wa DYCC, jijini Dar es Salaam.
“Sina shida kabisa na uongozi uliopo madarakani, wengi wao ni vijana wangu, lakini tatizo langu mimi ni katiba na namna inavyosimamiwa hapo ndio kunavyonitatiza,” alisema Magoma na kuongeza:
“Siku ile katika ule mkutano tuliokuwa tunabadilisha katiba kama mtakumbuka nilinyoosha mkono, ili watu waelewe vizuri hoja yangu badala yake wakanikatalia kuuliza swali. Hii katiba baada ya mabadiliko yale, viongozi walipokwenda kuibadilisha ilitakiwa irudi kwetu tena wanachama ili tuulizwe kwa kupewa haki yetu, badala yake wakafanya wanayoyajua wao.
“Viongozi wa Yanga wajitathimini sana katika hili, katiba ni kitu muhimu kwa maisha ya klabu au taasisi, watoe nafasi ya watu kukubaliana na sio kufanya mambo kwa kuharakisha.”
Magoma alisema aliamua kukaa kimya kwa muda mrefu, licha ya kuwa na hukumu hiyo akitanguliza busara kwa Yanga ili warekebishe hayo, mambo.
Kwa upande wa Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo, Evordy Kyando alipoulizwa juu ya sakata hilio, alisema hana taarifa rasmi kuhusiana na hukumu hiyo ya Mahakama ya Kisutu dhidi ya uongozi wa Yanga.
Kyando alisema, yeye amekuwa akifuatilia sakata hilo kupitia vyombo vya habari tu. “Siwezi kuzungumzia suala hilo kutokana na ukweli kuwa halipo rasmi kwangu, mimi pia nasoma na nasikiliza kupitia vyombo vya habari. Nitaangalia kwenye mafaili yangu kujua undani wake, kwa sasa sina jibu kamili kuhusiana na sakata hilo,” alisema Kyando.
Kwa upande wa Msemaji wa Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (RITA), Jafari Malema hakuweza kuzungumzia suala hilo, huku akitoa maelekezo kwa huduma ya kupata taarifa za masuala ya ufafanuzi utolewa kwa kuandika barua na kuomba upekuzi wa taarifa za wadhamini ambapo utalipia.
“Pia unaweza kwenda katika klabu husika kuomba kupatiwa status ya wadhamini waliopo kwa sasa. Pia fika ofisini RITA makao makuu utakutana na wahusika. Kwa sasa nipo mkoani kikazi,” alisema Malema.
Mwanasheria wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Herman Kidifu alisema hawezi kuzungumzia kinachoendelea mtandaoni kwa sasa, bali anasubiri hukumu inayohusu Yanga imfikie ndipo atakuwa na nafasi ya kutoa ufafanuzi suala hilo.
“Hatujapokea hukumu hiyo inayowahusu Yanga hatuwezi kuzungumzia juu ya suala hilo na endapo tukipata Ofisa Habari wa TFF atatoa taarifa juu na suala hilo,” alisema Kidifu, huku mmoja wa viongozi wa soka ambaye hakutaja jina lake litajwe gazetini akiwashauri viongozi wa Yanga kufanya haraka kwa kuitisha mkutano mkuu na kulipa kipaumbele suala hilo ili kurudisha uhalali wake.
Alisema kwa mujibu wa walalamikaji hawakupeleka mahakamani klabu, bali walilishtaki Baraza la Wadhamini wa klabu hiyo, lakini athari yake ni kubwa kwani inaathiri klabu kwa ujumla.
“Uongozi usinyamaze kimya, uchukue suala hilo na kulifanyia kazi kwa kurudisha uhalali wake, waitishe mkutano mkuu wazungumze na kufanya maamuzi mengine ambayo yataiweka klabu kwenye uhalali,” alisema kiongozi huyo:
“Sababu kubwa ya wanachama ambao kikatiba wamekiuka kutokana na kupeleka keshi hiyo mahakamani na sio kuipeleka kwenye mahakama za mpira ambazo ni kamati ya nidhamu na maadili kwa mujibu wa timu zetu.”
Alisema sababu ya klabu kukatazwa kupeleka masuala ya soka mahakamani ni kutokana na kesi zake kuchukua muda mrefu, hivyo kusababisha kuwamisha maendeleo ya soka.
“Sababu kubwa ya wanachama hao kupeleka mahakamani nafikiri ni kutokana na kuamini kuwa haki yao haitasikilizwa, na sio hivyo, kitendo walichokifanya wamevunja katiba ya klabu ingawa ni haki ya msingi ya katiba ya nchi inamruhusu kwenda mahakamani, lakini sio kila jambo kwenda mahakamani,” alifafanua.
Akizungumzia anachokiona mara baada ya wanachama hao kupeleka kesi mahakamani juu ya viongozi walio madarakati kutotambulika na watatakiwa kung’oka ikiwamo kuhusu kufungiwa, alisema hafikirii kama itafikia huko.
Katika mitandao ya kijamii wadau mbalimbali wa soka wamekuwa wakitoa maoni, huku wakielekeza lawama kwa wanachama waliofungua kesi wakidai wanataka kuipelekea Yanga katika maisha ya ombaomba baada ya kuona neema na mafanikio yamerejea kiasi kwamba klabu hiyo imerejesha ufalme ilioupoteza.
Yanga ipo kwenye mchakato wa kutaka kuigeuza klabu hiyo kuendeshwa kama kampuni kupitia hisa kama ambavyo Simba imekuwa ikipambana kufanya,hivyo licha ya sasa kumtambulisha Mohammed Dewji kama mwekezaji kabla ya mchakato haujakamilika akitajwa atamiliki hisa asilimia 49 na zilizosalia ni za wanachama.