179 mbaroni Mwanza, yumo anayedaiwa kumuua mwanamke

Mwanza. Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza linawashikilia watu 179 akiwemo Mkazi wa Nyakasela Kata ya Nyakariro Sengerema mkoani Mwanza, Lupande Ng’wani (43) anayedaiwa kumuua Mwajuma Yugele kwa kumpiga na kitu kizito kichwani.

Taarifa hiyo imetolewa leo Alhamisi Julai 18, 2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wibroad Mutafungwa, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema mtuhumiwa wa mauaji anadaiwa kutenda kosa hilo kwa kile kinachotajwa kuwa ni wivu wa mapenzi.

“Mauaji hayo yalitokea Julai 17, 2024, Saa 11 alfajiri katika Kijiji cha Nyakasela, baada ya kufanya upelelezi wa kina kufanyika tulifanikiwa Julai 16, mwaka huu Saa 2:00 asubuhi, tulimkamata Lupande akiwa amejificha Kijiji cha Bugango Wilaya ya Msalala mkoani Shinyanga,” amesema Kamanda Mutafungwa.

Amesema wengine waliokamatwa ni kundi la uhalifu la watu 39 waliokamatwa na kilo 14.2 za bangi, 63 wamekutwa na lita 134 za gongo na mitambo mitano ya kutengeneza pombe hiyo.

Pia, amesema watuhumiwa 63 wamekutwa na vifaa vya kupigia ramli chonganishi na watuhumiwa wawili wakikamatwa kwa kukutwa na mashine aina ya ‘Injector Pump’ ya mtambo unaotumika kutengenezea barabara huku uchunguzi ukiendelea kujua uhalali wake.

“Pia tumekamata vielelezo vikiwemo deki tatu, pikipiki tano aina ya TVS, SUNLG, bajaji na KingLion mbili, mali zote hizo zinadhaniwa kuwa ni za wizi,” amesema Mutafungwa.

Katika hatua nyingine, jeshi hilo limezindua ‘Wiki ya Nenda kwa Usalama’ kwa kuendesha ukaguzi wa magari wa lazima ambapo magari 275 ya shule binafsi yamekaguliwa mkoani humo kuanzia Julai Mosi mwaka huu, 234 yalikutwa yakiwa hayana hitilafu huku magari 41 yakikutwa na ubovu.

“Baada ya ukaguzi wamiliki wa waliamriwa kwenda kuyatengeneza na kuyarejesha kituoni kwa ajili ya ukaguzi. Madereva 275 walipewa elimu ya usalama barabarani sambamba na kukaguliwa leseni zao, tumejipanga kufanya ukaguzi wa lazima kwa vyombo vya moto,” amesema.

Kuhusu magari yaliyokaguliwa, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mwanza, Sunday Ibrahim amesema wanaobainika kuwa na vyombo vya moto visivyo na dosari watatakiwa kulipia Sh2,000 (pikipiki), Sh5,000 (magari binafsi) na Sh7,000 (magari ya abiria), fedha inayolipwa kwenye ‘control’ namba ili kuwekewa stika maalumu ya ukaguzi huo.

Ibrahim ameonya wenye magari watakaokaguliwa kuepuka utapeli kwa kwa kukabidhi fedha taslimu baada ya kukaguliwa vyombo vyao, badala yake amesisitiza wamiliki wa vyombo hivyo kuvifikisha katika vituo vya polisi na stendi kwa ajili ya ukaguzi kisha kulipia kwa kutumia ‘control’ namba kisha kupatiwa risiti.

“Ukaguzi huu unajumuisha leseni na ubora wa chombo, hatutocheka na dereva ama mmiliki wa chombo chochote kwa hiyo tunawataka kuleta vyombo vyao maeneo ya ukaguzi kabla hatujakufikia. Tunafanya hivi ili kuondoa ajali zinazotokea lakini zingeweza kuzuilika,” amesema Ibrahim.

Related Posts