Sengerema. Wakazi 296,410 mkoani Mwanza, watanufaika na mawasiliano ya simu baada ya Serikali kujenga minara 17 itakayoongeza mawasiliano kwenye kata 16 na vijiji 52 vilivyoko ndani ya mkoa huo.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi Julai 18, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda alipokuwa akisoma taarifa ya mkoa kwenye ziara ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nauye, alipokuwa wilayani Sengerema.
Amesema kwa sasa Mkoa wa Mwanza una minara ya simu 422 inayotoa mawasiliano na ongezeko la minara 17 inayojengwa sasa, itaboresha mawasiliano ya wananchi hususan wa vijijini.
Leo, Waziri Nape anatembelea mnara wa simu ulioko Kisiwa cha Lyakanyasi kilichopo Kata ya Chifunfu, Wilayani Sengerema.
Katika kuhakikisha minara hiyo inajengwa na kutoa huduma kwa wananchi, Serikali inatoa ruzuku ya Sh2.44 bilioni kwa makampuni ya simu ili kuwezesha kampuni za simu kujenga minara hiyo.
Hata hivyo, imeelezwa kuwa Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imetoa ruzuku ya Sh2.44 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa minara 17 mkoani Mwanza kwenye mradi wa ujenzi wa minara 758 katika mikoa 26 ya Tanzania Bara.
Ujenzi wa minara hiyo 17 itanufaisha kata 16, vijiji 52 huku wananchi 296,410 wanaoishi vijijini ambao watanufaika na huduma ya mawasiliano mkoani humo.
Mtanda amesema hadi kufikia mwishoni mwa Juni 2024 jumla ya minara 7 imewashwa mkoani humo na inatoa huduma ya mawasiliano kwa teknolojia ya 2G, 3G na 4G.
Amesema vijiji ambavyo vimeanza kunufaika ni vya Kata ya Nyamhongolo, Sangabuye, Shibula, Kandawe, Lubili, Chifunfu na Igalula.
Leo ikiwa ni siku ya nne ya ziara ya Waziri Nape katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kukagua ujenzi wa minara 758 inayojengwa katika mikoa 26 ya Tanzania Bara na zaidi ya wanakijiji milioni 8.5 nchini watanufaika na mradi huo.
Akizungumza leo, Nape amesema azma ya Serikali ni kuona inamaliza changamoto ya mawasiliano hasa maeneo ya vijijini.
Hivyo, amewataja watendaji wa Serikali kusimamia minara hiyo iliyojengwa kama wanavyosimamia sekta zingine.
“Tunataka mawasiliano kwa wananchi yalete matokeo chanya, yawasaidie kupata maendeleo kwenye maeneo yao,” amesema Waziri Nape.
Mwananchi imezungumza pia na baadhi ya wananchi wilayani Sengerema ambao wameiomba Serikali kuzihamasisha kampuni za simu kujenga minara kwenye maeneo yao.
Jumanne Juma, mkazi wa Sengerema amesema mawasiliano ya simu za mkononi yanapoboreshwa, yanasaidia wananchi kupata maendeleo.
Mbunge wa Sengerema, Hamis Tabasamu, ameishukuru Serikali kwa kujenga minara hiyo ambayo sasa inakwenda kutatua shida ya mawasiliano ilyokuwapo kwa muda mrefu.
Hata hivyo, amemuomba Waziri Nape, kuwa kuna kata nne kati ya 26 zinazounda Halmashauri ya Sengerema, bado zina tatizo la mawasiliano, hivyo amemuomba ikiwezekana zipate minara haraka.
Amezitaja kata hizo ni pamoja na ya Kishinda, Buyagu na Bitoto, alikosema wakazi wake wanapata mawasiliano kwa shida.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Sengerema, Marco Makoye amesema Wilaya ya Sengerema ina visiwa zaidi ya 28 hivyo kuweka minara ya simu kwenye maeneo hayo itawasaidia sana wananchi.