Mwanza. Daniel Sayi (48) mfanyabiashara wa ng’ombe wilayani Geita mkoani hapa, anadaiwa kuchukuliwa na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake Kitongoji cha Kiomboi, Kijiji cha Ihilika, Kata ya Nyarugusu mkoani Geita.
Sayi inadaiwa alichukuliwa Mei 13, 2024 saa 12 jioni baada ya watu wanne waliokuwa na gari aina ya Toyota Land Cruzer yenye rangi nyeupe kufika nyumbani kwake na kumfunga pingu kisha kumchukua bila kusema chochote ikiwa sasa ni miezi miwili.
Kwa mujibu wa familia ya Sayi, tangu achukuliwe nyumbani kwake wamehangaika vituo mbalimbali vya polisi kikiwamo cha Nyarugusu, Katoro na Geita lakini hawajafanikiwa kumpata na hawajui waliomshikilia ni kina nani.
Kutokana na kutoweka kwa ndugu yao tayari wametoa taarifa polisi na kupewa RB namba NGS/RB/230/2024 iliyotolewa kituo cha Polisi Nyarugusu.
Michael Daniel, ambaye ni mtoto wake, amesema siku ya tukio, Mei 13, 2024, wakiwa na baba yao nyumbani, gari hilo lilifika na wanaume wanne wakashuka.
Kisha dereva akaliendesha hadi mbele kidogo akageuza na kwenda kuliegesha jirani na nyumba yao.
Michael anasema alikuwa amekaa kibarazani na baba yake alikuwa amekaa ndani anaangalia mpira kwenye runinga na aliposikia anauliziwa, akatoka nje.
Anasema alidhani ni marafiki zake japo alikuwa hajawahi kuwaona hata mara moja.
“Walifika wakanikuta nimekaa hapo nje barazani na baba alikuwa kwenye nyumba kubwa anaangalia mpira, aliposikia watu wanamuulizia alitoka nje walipomuana tu walimfuata na kumfunga pingu bila kusema chochote, wakamchukua na kumuamrisha apande kwenye gari na wakati huo gari ilikuwa imeshaegeshwa kwenye geti,” amesema Michael.
Baba wa Daniel, mzee Elias Sayi Mkazi wa Simiyu, amesema baaada ya kupata taarifa ya mtoto wake kukamatwa alijua amekamatwa na polisi na kuagiza ndugu zake wengine kwenda polisi kujua kosa lake kwa kuwa hakuwahi kusikia mwanawe akihusishwa na matukio ya uhalifu.
“Mwanagu anajishughulisha na kilimo na biashara ya kunua ng’ombe wakikua baada ya mwaka anawauza, sijawahi kupokea malalamiko yoyote lakini baada ya kukamatwa tumehangaika kumtafuta bila mafanikio,” amesema mzee huyo alipozungumza na Mwananchi.
Baba huyo amedai Daniel ni mwanaye pekee wa kiume ambaye alikua akimtegemea, lakini sasa analazimika kuwatunza watoto 23 wa Daniel ambao bado ni wadogo na wanamhitaji baba yao.
“Hapa tuko kwenye kifungo hatujui hatma maana angekua ameugua na kufa tungezika na kuona kaburi lake, lakini sasa hivi nyumba iko kama inamsiba, mwili haupo na hatuwezi kufanya chochote tunaiomba sana Serikali namuomba Rais Samia (Suluhu Hassan) yeye ni mzazi kama mimi anisaidie nimpate mtoto wangu,” amesema Sayi.
Ibrahim Masanja baba mdogo wa Daniel amesema wamefanya jitihada za kumtafuta kwa kwenda polisi na ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Geita kujua aliko ndugu yao bila mafanikio.
“Tumetoa taarifa kila mahali tunachoambiwa ni kusubiri tumesubiri miezi miwili sasa lakini hatunajapewa mrejesho, polisi wanasema hawajui aliko sasa tunajiuliza nani walimchukua tumepewa mpelelezi lakini hata nyumbani hajafika,” amesema.
Masanja ameomba wanaomshikilia kumpeleka mahakamani ili wajue makosa anayoshtakiwa nayo badala ya kuwa kimya wakati hawajui ndugu yao aliko.
Amesema Daniel mwenye watoto 23 na wake watatu, familia yake imeathirika kisaikolojia na kuiomba Serikali kusaidia ili ndugu yao apatikane.
Salome Nyasika mke mkubwa wa Daniel, amesema maisha ya nyumbani yamekuwa magumu kwa kuwa mume wake ndiye aliyekuwa akitegemewa kuendesha familia.
Hata hivyo, alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Sophia Jongo kuzungumzia tukio hilo alisema anaifuatilia taarifa hiyo kujua undani wake.
“Nataka nifuatilie waliliripoti kituo gani na lini? wakati mwingine kuna kuwa na changamoto mtu anaweza kuripoti akipotea lakini akipatikana harudi tena kumbe alitoka tu na mambo yake wao wanaona ayupo.
“Ndiyo maana nasema ngoja niifuatilie,” amesema.
Mwananchi Digital imefika ofisini kwake leo Julai 18, 2024 na haikufanikiwa kumpata kutokana na kutokuwa ofisini na hata alipopigiwa simu haikupokewa jitihada za kumtafuta zinaendelea.