DODOMA Jiji imemsainisha kiungo wa ushambuliaji Ibrahim Ajibu kwa mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia timu hiyo msimu ujao akitokea Coastal Union ya Tanga.
Mmoja wa viongozi wa timu hiyo ameliambia Mwanaspoti kwamba bado wanaamini Ajibu ana uwezo mkubwa uwanjani hivyo ataongeza nguvu katika kikosi chao.
“Usajili huo unafanywa chini ya kocha Mecky Maxime, ambaye anawafahamu vyema wachezaji wazawa kwani amecheza na kufundisha timu mbalimbali kwa muda mrefu.
Ameongeza: “Ajibu ataungana na wachezaji wengine kambini tayari kwa maandalizi ya msimu ujao na bado hatujakamilisha usajili tunaendelea kumalizia wengine waliobakia ambao tupo nao kwenye mazungumzo ya mwisho.”
Kiongozi huyo anaamini kikosi cha Dodoma Jiji msimu ujao kitakuwa na ushindani mkubwa kutokana na aina ya wachezaji ambao wanawachukua akiwemo Ajibu na Joash Onyango anayejiunga nao kwa mkopo.
Klabu hiyo pia imewanyakua Dickson Mhilu na kipa Alain Ngeleka kutoka Kagera Sugar na Reliants Lusajo kutoka Mashujaa aliyepewa mkataba wa miaka miwili.