KOCHA David Ouma alifanya kazi nzuri na ya kipekee katika kikosi cha Coastal Union msimu uliopita tofauti na matarajio ya wengi.
Jamaa aliikuta Coastal Union inayosuasua kwenye Ligi, lakini ndani ya muda mfupi akaibadilisha na ikaanza kufanya vizuri hadi kufanikiwa kumaliza katika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu Bara msimu uliomalizika.
Coastal ambayo katika msimu wa 2022/2023 ilikuwa na safu dhaifu ya ulinzi iliyoruhusu nyavu kutikiswa mara 35, ikawa na ukuta wa chuma katika msimu uliomalizika ambayo ilifungwa mabao 19.
Na bahati ikawaangukia baada ya Yanga ambayo imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu kuchukua Kombe la TFF, wao Coastal wakapata fursa ya kuiwakilisha Tanzania katika Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.
Huwezi ukayatenganisha mafanikio hayo na uwepo wa David Ouma ambaye uongozi wa Coastal uliamua kubaki naye kwa vile aliweza kuwaimarisha wachezaji mmoja mmoja na timu kiujumla.
Sasa kushiriki kwa Coastal katika Kombe la Shirikisho Afrika na pia kupigania muendelezo wa kumaliza katika nafasi ambayo wamemaliza msimu uliopita ni mambo mawili ambayo yanaweza kufanya uthibitisho wa ubora wa kocha Ouma.
Kwanza ni kwa sababu Coastal haina uzoefu mkubwa na mashindano makubwa barani Afrika hivyo Ouma kama kocha anapaswa awaandae vyema kisaikolojia ili waweze kufanya vizuri.
Lakini anawakosa baadhi ya wachezaji tegemeo ambao waliibeba timu hiyo msimu uliopita uliomalizika mfano wa mabeki hao ni Ferry Mulumba na Lameck Lawi kwa sababu tofauti. Lawi akienda kucheza soka la kulipwa Ubelgiji na Mulumba yeye ameachwa.
Hapo tunataka kuona uwezo wa Ouma wa jinsi gani anavyoweza kutengeneza wachezaji hadi akafanikiwa kupata kama kile cha msimu uliopita au zaidi ya hapo na pia akaiwezesha itambe katika mashindano ya ndani.