Biashara yazidi kuimarika mpaka wa Tunduma

Dar es Salaam. Mpaka wa Tunduma- Nakonde umetajwa kuwa kichocheo kikubwa cha biashara kati ya Tanzania, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), huku takwimu zikionyesha biashara katika eneo hilo ikiongezeka maradufu.

Mafanikio hayo yameonekana ikiwa imepita miezi tisa baada ya Tanzania na Zambia kukubaliana kuzifanyia kazi changamoto nane kati ya 24 za kibishara, ikiwemo kupunguza msongamano wa malori katika mpaka huo.

Akizungumza leo Alhamisi Julai 18, 2024 wakati msafara wa Rais Samia Suluhu Hassan uliposimama wilayani Tunduma, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile amesema changamoto ya foleni ya malori ni matokeo ya maboresho yaliyofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam.

Amesema maboresho hayo yanachangia kuongezeka kwa mzigo unaopita kwenye mpaka wa Tunduma ambao kwa kiasi kikubwa umeongeza mapato katika nchi.

“Hakuna jema linalokuja bila kuwa na changamoto, mwaka 2022 malori yaliyokuwa yanapita hapa yalikuwa 124,000 kumefanyika maboresho mbalimbali ya kibiashara pamoja na bandarini, hali iliyosababisha malori kuongezeka hadi kufikia 261,000.

“Mzigo umeongezeka kutoka tani milioni 3 hadi tani milioni 6.2 milioni. Hii imesababisha makusanyo kuongezeka kutoka Sh76 bilioni hadi Sh159 bilioni,” amesema.

Naibu Waziri Kihenzile amesema kabla ya maboresho ya bandari, mzigo uliokuwa unakwenda Zambia ulikuwa tani milioni 1.1, sasa ni tani milioni 2.2 wakati mzigo wa Congo ulikuwa tani milioni 1.9, lakini sasa imefika tani milioni nne.

Pamoja na mafanikio hayo, ameeleza bado kuna maeneo yanaendelea kufanyiwa kazi, ili kumaliza changamoto ya foleni, eneo mojawapo ikiwa ni kuwezesha kupatikana kwa scanner ya kisasa upande wa Zambia.

“Upande wetu uko vizuri, ila upande wa pili una changamoto, umeidhinisha Sh11 bilioni tupo katika hatua za mwisho kununua, ili kazi ifanyike kwa ufanisi. Changamoto nyingine ni kutosomana mifumo kati ya upande wa Zambia na TRA, vikao bado vinaendelea na muda si mrefu vitahitimishwa na mambo yatakaa sawa,” amesema.  

Akiwasilisha kilio cha wananchi, Mbunge wa Momba (CCM), Condester Sichalwe amelalamikia changamoto katika upatikanaji wa Vitambulisho vya Taifa katika Mkoa wa Songwe.

Mbunge huyo ameeleza wananchi wa Songwe wamekuwa wakilalamika kutopata vitambulisho vya Taifa vinavyotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), hivyo kukwama kupata baadhi ya huduma muhimu.

Ameshauri vitambulisho hivyo vinaweza kutolewa sambamba na uandikishaji wapigakura kwenye eneo hilo, ili kurahisisha maisha ya wananchi wa Tunduma na mkoa mzima wa Songwe.

“Ombi langu kwako mama, wakati tutakuwa tunazindua daftari la wapigakura, tunaomba waandikishe na vitambulisho vya Nida. Kuna watu wa Tasaf wanashindwa kupata huduma kwa sababu ya vitambulisho hivyo,” amesema Sichalwe.

Akijibu changamoto hiyo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo, hasa kwa wananchi waishio pembezoni na kueleza tatizo hilo litakwisha kutokana na mipango iliyopo.

Amesema wakati Rais Samia anaingia madarakani, alikuta deni la mkandarasi la Sh7.5 bilioni, lakini amelipa zote. Alisema Serikali imetoa Sh2.5 bilioni kwa ajili ya kununua kadi zinazowatosha Watanzania wote nchini na tayari nyingine zimepelekwa Songwe.

“Maeneo ya mipakani yana mwingiliano mkubwa na watu wa nchi jirani. Hivyo unafanyika uhakiki wa raia, ili tujue nani anapewa kitambulisho. Hili ni muhimu kwa usalama wa Taifa,” amesema Masauni.

Hata hivyo, amesema Serikali imezindua mkakati maalumu wa utoaji vitambulisho kwa wananchi waishio mipakani na kwamba mambo yatakuwa mazuri yakifanyika mabadiliko ya mfumo wa utendaji wa Nida.

“Tumeanza kuzitatua changamoto hizo hatua kwa hatua. Mtakumbuka Rais alitupa ushauri wa kuwa na namba moja ya utambulisho wa Mtanzania. Mambo haya ni muhimu kuyafanyia utafiti kuangalia muundo na utendaji kazi wa Nida kwa ujumla wake.

“Mambo haya yanahitaji mabadiliko ya sheria. Kamati iliyokuwa kazini, imemaliza kazi yake. Tunataka chombo hiki kifanye kazi yake kwa ufanisi, ili kupunguza malalamiko ya wananchi,” amesema Waziri Masauni.

 Akiwasalimia wananchi wa Mlowa wilayani Mbozi, Rais Samia ametoa msisitizo kwenye kukata bima ya afya kujihakikisha matibabu. 

“Mnajua maendeleo yakifanywa huzaa changamoto nyingine, mmeshuhudia Serikali imejenga hospitali za aina zote sasa na zina vifaa vya kisasa, ili kuzuia wananchi wasilazimike kwenda nje ya nchi kufuata matibabu. 

“Matibabu haya yana gharama na ili tuwe na mfumo mzuri wa kutoa huduma ni lazima tuchangie huduma za afya, hapa nazungumzia bima ya afya. Sisi ni wakulima, wachimba madini wazuri, basi tuwe na utaratibu wa kutenga kiasi kidogo cha fedha ukanunue bima ya afya ili kuepuka usumbufu wa kupata vipimo na kutibiwa maradhi yanapokuja,” amesema.

Related Posts