Bosi TRA atoa mwelekeo mpya, awatahadharisha wafanyabiashara

Dar es Salaam. Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda amewaahidi viongozi wa sekta binafsi ushirikiano, kuboresha huduma kwa wateja, kushughulikia watendaji wanaochafua taswira ya TRA, kupanua wigo wa kodi na kuweka kodi himilivu pamoja na kufanya maboresho mfumo wa kodi.

Mbali na hayo, amesema uteuzi wake hautabadilisha kitu chochote katika utendaji wa TRA na badala yake ataendeleza yale ambayo tayari yamefanywa na mtangulizi wake na kuongeza mapya.

Julai 1, 2024, Rais Samia Suluhu Hassan, alifanya uteuzi wa Mwenda kuwa bosi mpya wa TRA akichukua nafasi ya Alphayo Kidata aliyeteuliwa kuwa mshauri wa Rais Ikulu. Awali, Mwenda alikuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA).

Leo Alhamisi, Julai 18, 2024, Mwenda amefanya kikao cha kwanza kati ya timu ya ofisi yake na viongozi wa sekta binafsi ikilichoandaliwa na Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

Pia, mkutano huu unafanyika ikiwa ni siku chache tangu mgomo wa Kariakoo, Dar es Salaam na mikoa mingine kama Dodoma, Kigoma, Mbeya, Mwanza, Iringa na Morogoro kufikia tamati ambao pamoja na sababu nyingine kodi na kamatakamata inayofanywa na TRA ilikuwa sababu.

Mwenda amesema kitu cha kwanza atakachofanya katika kuendeleza yale yaliyofanywa na mtangulizi wake Kidata atahakikisha ushirikiano na kuboresha huduma kwa wateja.

“Nikiwa kama kiongozi mkuu wa taasisi nitaimarisha ushirikiano kati ya TRA na wafanyabiashara wote chini ya vyama vyao,” amesema Mwenda.

Amesema kama kiongozi atahakikisha anaimarisha huduma kwa wateja ili kupunguza malalamiko yanayokuwapo.

“Na katika hili, nilitaka ikiwezekana kila robo ya mwaka tukutane tupate mrejesho ya tuliokubalinana na kuangalia tunaendaje mbele kwa lengo la kuboresha ufanyaji biashara ndani ya nchi,” amesema Mwenda.

Wakati hilo likifanyika amesema watumishi ambao wanaichafua TRA watashughulikiwa ili kifanya biashara zifanyike katika hali ya utulivu na usawa.

Amesema kama watu wakishindwa kufanya biashara ni ngumu kukusanya kodi na hilo linawezekana ikiwa watakaa pamoja kuzungumza kwa pamoja na kupata namna ya kwenda mbele.

“Nimeona mengi yanayoendelea tunao ujuzi na watu wenye utaalamu lakini maboresho yanahitajika kila siku tutaendelea kuwapa mafunzo ili wafanye kazi kwa weledi kwani tunaongozwa na sheria,” amesema Mwenda.

Amesema kama kiongozi pia atasimamia mamlaka ya sheria aliyopewa panapohitajika kwa ajili ya maamuzi ya mapato.

“Wafanyabiashafa wengi ni wazuri na bado wachache ambao hawatekelezi matakwa ya sheria kama kukwepa kodi, bodhaa bandia, dumping ya mizigo zinakuja kwenye soko kushindana na watu wanaofuata njia sahihi.

Kwa pamoja tutafute njia ya kuzuia kwa sababu kodi na usimamizi wa kodi si tu kukusanya hata kusimamia shughuli za kiuchumi,” amesema.

Amesema ikiwa jambo hili litasimamiwa kwa ushirikiano na wafanyabiashara na wao kufuata masharti vizuri inaweza kusaidia kupunguza mzigo wa kodi hata Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na utitiri wa kodi na tozo.

Kuhusu kutanua wigo wa walipa kodi jambo ambalo limekuwa likipigiwa kelele na wafanyabiashara wengi ameahidi kulifanyia kazi baada ya kukaa kwa pamoja na sekta binafsi.

“Tutakaa pamoja kuangalia namna ya kuongeza walipa kodi ili kupunguza mzigo wa kodi kutoka wale wachache wa sasa,” amesema Mwenda.

Katika hatua nyingine, amesema wafanyakazi wasiokuwa watiifu watawashughulikia kwani baadhi walipewa nafasi ya kujirekebisha huku akitoa rai kwa wafanyabiashara kuacha kuwashawishi kupokea kodi.

“Rushwa inatoka kwenu pia mnawashawishi baadhi ya watu ili mkwepe kodi mkifanya hivyo mnaharibu hii taasisi, kama mtu hajalipa kodi na deni ni kubwa sheria inaruhusu kuzungumza kulipa kidogokidogo,” amesema Mwenda.

Katika hilo amesema hakuna mtu mwenye nguvu ya kukusamehe kodi kwa sababu ya nguvu aliyopewa anaweza kuhairisha akafanya kama hajaiona lakini baadaye atarudi kulekule.

“Pia, tutaboreaha mfumo wetu wa kodi, tutafanya ushirikiano na Wizara ya Fedha kutoa mapendekezo ni jinsi gani tunaweza kuboresha mfumo wetu wa kodi,” amesema Mwenda.

Related Posts