Chama mambo freshi Yanga | Mwanaspoti

KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Clatous Chama sasa mambo freshi kuendelea kuitumikia timu hiyo ambayo imemsajili akitokea kwa watani zao, Simba.

Chama amejiunga na Yanga kwa mkataba wa mwaka mmoja na tayari anaendelea na maandalizi ya kujiweka fiti kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Bara unaotarajia kuanza Agosti 16, mwaka huu.

Awali, Mwanaspoti liliripoti kuwa Chama hajamalizana na Simba kutokana na kushindwa kumpa barua ya kumuachia akiwa mchezaji huru, lakini sasa ni rasmi staa huyo mwenye rekodi Ligi Kuu Bara yupo huru kukipiga Jangwani.

Taarifa ambazo Mwanaspoti lilizipata zilibainisha Simba haikumpa Chama barua ya kumuacha licha ya kwamba nyota huyo amemaliza mkataba ndani ya kikosi hicho.

Juzi Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ilikutana kujadili mashauri yaliyowasilishwa, huku suala la Chama likionekana kutojadiliwa ndipo Mwanaspoti lilipomtafuta Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Said Soud aliyelitolea ufafanuzi suala hilo ambapo alisema halikujadiliwa kwa sababu liliisha kabla ya kikao hicho.

“Ni kweli jana (juzi) hakukuwa na mjadala kumhusu kiungo huyo sababu ni kwamba licha ya Yanga kuleta malalamiko yao, changamoto hiyo ilitatuliwa kabla ya kikao chetu cha jana (juzi),” alisema.

“Yanga ndio walileta malalamiko kuhusiana na suala hilo kuhusu kwanini halikujadiliwa. Bafikili sababu ni kutatuliwa kabla ya kikao ambacho tumekifanya jana (juzi).”

Akizungumzia suala la kuondolewa kwenye shauri linalomhusu beki Lameck Lawi dhidi ya Simba, Soud alisema ni uamuzi wake kutoka lakini haihusiani na yeye kuwa na uhusiano wa karibu na Coastal Union.

“Ujue inaripotiwa tofauti watu wanazungumza kwamba niliondolewa sio kweli kamati iliridhia mimi kuendelea kuwepo kwenye kesio hiyo lakini mimi binafsi niliomba kuondoka ili kutoa uhuru wa kujieleza kwa wapinzani,” alisema.

“Kesi ya Lawi naina tofauti na ya Feisal Salum ‘Fei Toto’ kipindi hicho kabla ya kuanza kuitumikia Azam FC kwenye kamati kulikuwa na Alex Mgongorwa ambaye ni mwanachama wa Yanga, lakini kamati iliridhia kumuacha asikilize kama ilivyokuwa kwangu pia lakini mimi niliomba kutoka sikutolewa.”

Simba inailalamikia Coastal kuvunja makubaliano ya mauzo ya Lawi, shauri lililosikilizwa TFF sambamba na lile la Francy Kazadi aliyeishtaki Fountain Gate kushindwa kumlipa chake.

Related Posts