DKT. MFAUME ATOA MAELEKEZO MAZITO KWA MAAFISA LISHE – MWANAHARAKATI MZALENDO

Mkurugenzi wa Huduma za Afya Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt.Rashid Mfaume amewaelekeza Maafisa Lishe wa Mkoa na Halmashauri nchini kuhakikisha wanaimarisha huduma za lishe ikijumuisha afua za Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ili kuwezesha makuzi kamilifu ya mtoto.

Akitoa maelekezo hayo Julai 17,2024 Jijini Dodoma wakati akifunga mkutano wa mwaka wa uratibu wa maafisa lishe wa mikoa na Halmashauri nchini Dkt. Mfaume amesema uimarishaji huo utasaidia watoto kukua kimwili na kiakili na kutengeneza kizazi chenye mchango wa maendeleo kwa Taifa.

Hata hivyo Dkt. Mfaume amewataka maafisa hao kubuni afua za lishe zinazojibu changamoto na visababishi vya udumavu kwenye maeneo yao ili kutatua sababu mahsusi za udumavu katika jamii husika.

Dkt.Mfaume amewataka kuhakikisha wanatoa elimu kwa jamii kuhusu kuboresha matunzo ya lishe kwa makundi maalumi ili kufifisha mila, desturi na imani potofu zinazochangia uwepo wa tatizo la lishe kwenye jamii.

“Suala la elimu ya lishe lizingatie pia afua za kudhibiti magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza ambayo tafiti zinaonesha kuwa yanauhusiano mkubwa na masuala ya ulaji wa chakula, lishe na mitindo ya maisha.”amesisitiza Dkt.Mfaume

Aidha amewataka kuhakikisha wanaratibu na kuisimamia fedha zinazotengwa kwa ajili ya afua za lishe ili ziweze kutumika kwa malengo yaliyowekwa.

Naye,Mwenyekiti wa wadau wa lishe Tanzania Dkt.Teddy Jumbe amesema kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali katika kutekeleza afua za lishe pamoja na kutafuta rasilimali fedha na wataalamu wa kusaidia katika masuala ya lishe nchini.

“Tutatumia utaalamu wetu wote kuhakikisha kwamba afua za Lishe zote ambazo zinatekelezwa hapa nchini ni afua mabazo zinatusaidia kama watanzania katika mazingira yetu ya kitanzania” amesema Dkt. Teddy Jumbe

Mkutano wa siku mbili wa mwaka wa uratibu kwa maofisa Lishe wa mikoa na Halmashauri nchini kwa mwaka 2024 uliokuwa umebeba kauli mbiu ya Uwajibikaji,Uratibu na Ubunifu ni nguzo kuu katika kuboresha huduma za Lishe nchini umehitimishwa Leo jijini Dodoma.

Cc:Tamisemi

#KonceptTvUpdatesImageImage

Related Posts