Kesi ya Malisa kizungumkuti, yakutwa haijasajiliwa

Moshi. Kesi ya uchochezi inayomkabili Mwanaharakati na Mkurugenzi wa GH Foundation, Godlisten Malisa imezua sintofahamu baada ya kufika mahakamani leo, Julai 18, 2024 mkoani Kilimanjaro na kukuta kesi hiyo bado haijasajiliwa.

Malisa akiongozana na mawakili wake watatu kati ya saba, wakiwamo Dickson Matata, Hekima Mwasipu na Peter Kidumbuo, walifika mahakamani hapo saa tatu asubuhi kama alivyotakiwa na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Kilimanjaro (RCO) kwa ajili ya kusikiliza kesi hiyo inayomkabili.

Wengine waliofika mahakamani hapo ni wafanyakazi wa taasisi yake, akiwamo James Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Michael Kilawila na marafiki zake wa karibu.

Malisa alikamatwa Juni 6, 2024 muda mfupi baada ya kesi inayomkabili yeye na Meya wa zamani wa ubungo, Boniface Jacob kuahirishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Jijini Dar es Salaam na kusafirishwa hadi mkoani Kilimanjaro akikabiliwa na tuhuma tatu.

Malisa anakabiliwa na tuhuma tatu, ikiwemo kuchapisha taarifa za uchochezi kuhusu mauaji ya Beatrice Minja, mkazi wa Rombo anayedaiwa kuuliwa na mtu aliyejulikana kwa jina la Paul Tarimo na tukio la mwanafunzi anayedaiwa kuuliwa kwa kichapo Moshi.

Tuhuma nyingine ni kutoa taarifa bila kibali kwenye akaunti yake ya Instagram kuhusu walimu waliokuwa wakisahihisha mitihani ya kidato cha nne Januari, 2024 kuhusu kutolipwa posho zao.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro, wamekiri kumfahamisha Malisa kuwa kesi yake itapandishwa mahakamani leo na kwamba kilichokwamaisha ni changamoto ya mtandao katika kusajili kesi hiyo.

Aidha, taarifa hiyo imesema Malisa atatakiwa kufika tena mahakamani hapo Julai 25, 2024.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi, Julai 18, 2024 akiwa katika viunga vya mahakama, Malisa amesema jana Jumatano Julai 17, 2024, wakili wake alipewa taarifa mteja wake atapandishwa mahakamani leo.

Amesema licha ya kutakiwa kufika mahakamani hapo leo, wameshangazwa na taarifa kuwa kesi hiyo bado haijasajiliwa, jambo waliloliona kama usumbufu na kupoteza muda kwa kuwa wameacha shughuli zao kwa ajili ya kufika kusikiliza shauri hilo.

“Sasa tulipata taarifa kwamba leo tuje mahakamani, wakili wangu akanijulisha, mimi nilikuwa nje ya nchi, nikalazimika kukatisha mkutano Nairobi nije hapa kusikiliza shauri langu, lakini tumefika leo shauri limeshindwa kusomwa, yaani Mahakama haina taarifa zetu, kwa lugha rahisi Mahakama inatushangaa,” amesema na kuongeza;

“Ikumbukwe tumetoka hapa Julai 11, ni juzi tu na kabla ya hapo tulisharipoti polisi mara tatu, hivyo katika kipindi cha mwezi mmoja tumesharipoti mara nne. Hii ni gharama, nakuja na jopo la mawakili kama mnavyowaona, mawakili wanaosikiliza kesi yangu wako jumla saba na leo wamefika hapa watatu,” amelalamika Malisa.

Hivyo, amesema hawatafika tena mahakamani hapo mpaka watakapoelezwa kuwa shauri hilo limesajiliwa na waitwe kwa oda ya Mahakama.

“Polisi watumie hekima na wawe waungwana kwa sababu hata ingekuwa ni wao, haiwezekani kila wakati unakuja kufuatilia shauri lile lile, lakini mtindo unakuwa ni ule ule njoo rudi njoo rudi. Fedha zinatumika, sisi hatuishi Moshi tunaishi Dar es Salaam,” amesema Malisa.

Akizungumzia mkwamo huo, mmoja wa mawakili wa mwanaharakati huyo, Hekima Mwasipu amesema mpaka wanaripoti leo mahakamani hapo walikuwa na uhakika mteja wao angepandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka yanayomkabili.

“RCO ndiye aliyepiga simu kwamba tunatakiwa Julai 18 hapa Kilimanjaro, tumefika leo asubuhi mahakamani, tumempigia simu kwamba tumeshafika, tukamuuliza twende ofisini kwake au mahakamani, akasema mahakamani hati ya mashitaka imeshasajiliwa, tumefika hapa mahakamani tunapiga simu hawapokei,” amesema wakili Mwasipu na kuongeza;

“Tunaambiwa hiyo hati ya mashtaka mtandao unasumbua kwa hiyo wanashindwa kuisajili, lakini mpaka tunakuja tulikuwa na taarifa za awali kwamba tayari hati ya mashtaka imeshasajiliwa na wakatuambia njooni mteja wenu asomewe hiyo hati ya mashitaka.”

Mwasipu amesema kwa mazingira hayo, hawatafika tena mahakamani hapo mpaka watakapopata taarifa za kujiridhisha kwamba hati hiyo imesajiliwa.

Wakili mwingine wa Malisa, Dickson Matata amesema; “Kimsingi sisi tunapokuja tunaripoti kwa RCO, taarifa hizi zimetolewa kwa RCO Kilimanjaro, sasa mahakamani hapa tumeambiwa hatuna kesi, Mahakama yenyewe inatushangaa maana haina taarifa yeyote.”

Amesema Julai 11, 2024 walikubaliana na polisi kwamba mteja wao afike kuripoti Julai 25, lakini walipigiwa simu kwamba asifike tarehe hiyo kuripoti, bali anatakiwa leo mahakamani.

“Tulitegemea upelelezi umekamilika na tayari hati ya mashtaka imeshaandaliwa na ipo mahakamani na kesi inaanza kusikilizwa, lakini mambo hayakuwa hivyo,” amesema Matata na kuongeza;

“Ndio maana leo tumekuja moja kwa moja mahakamani na hatujaenda kituo cha polisi, sasa tumekaa hapa tunasubiri kuitwa tunaambiwa hati ya mashtaka haijasajiliwa na leo mtandao ni mbovu. Hii si haki.”

Related Posts