Kibu azua utata Simba | Mwanaspoti

WAKATI Willy Onana na nyota mpya aliyetambulishwa juzi, Awesu Awesu jana walipaa kwenda kuongeza mzuka katika kambi ya Simba iliyopo, Ismailia Misri, nyota wa timu hiyo, Kibu Denis amezua utata.

Awesu na Onana ni kati ya wachezaji waliondoka nchini jana sambamba na baadhi ya viongozi kwenda Misri kuungana na wachezaji wengine wanaoendelea kujifua chini ya kocha mpya Fadlu Davids, lakini Kibu akiwa haonekani kambini na taarifa ni bado yupo Marekani akiendelea kula zake bata na familia.

Awali Simba kupitia chanzo kilichopo kambini, kilililiambia Mwanaspoti Kibu alikuwa ameshatua huko, lakini ukweli umebainika, walikuwa wanaficha, ila nyota huyo alikuwa hajaenda tofauti na taarifa hizo zilizotolewa wiki iliyopita na kuzua mijadala mtandaoni hadi sasa.

Mwanaspoti ilidokezwa mapema wiki hii, Kibu aliyemaliza na bao moja na aliyeongezwa mkataba hivi karibuni baada ya kuhusishwa na Yanga, angekuwa mmoja wa wachezaji ambao wangeondoka jana kwenda Misri, lakini hakuwepo katika msafara na kulazimika kudodosa kinachoendelea kwa mchezaji huyo.

Hata hivyo, imeelezwa Kibu bado hajarejea nchini akiendelea kula bata Miami Beach, iliyopo Jiji la Florida na haijawekwa wazi kitu gani kinachomfanya ashindwe kuungana na wenzake kambini kwani wachezaji wote wakiwamo wapya na wa zamani wameshaungana pamoja ukimuondoa Aishi Manula.

Katika kudodosa taarifa za Kibu, mtu wa karibu na mchezaji huyo aliliambia Mwanaspoti, ana ruksa maalumu, kwani alimaliza Ligi Kuu msimu uliopita akiwa majeruhi, hivyo anaendelea kujiuguza kabla ya kuja kuungana na wenzake.

“Ni kweli hajaenda kambini, ila ana ruksa maalumu kwa vile aliumia kabla ya msimu kumalizika na anajiuguza na viongozi wamekuwa wakiwasiliana naye, lakini bado hajapona, hivyo hata akienda huko hatakuwa na la kufanya, lakini utafute uongozi utakupa majibu zaidi,” kilisema chanzo hicho.

Kibu mwenyewe alipotafutwa ili kutoa ufafanuzi huo wa kukosekana kwake kambini, hakuwa tayari kusema lolote akitaka watafutwe viongozi. “Sina la kusema, we watafute viongozi,” alijibu Kibu kwa kifupi na Mwanaspoti lilipomsaka Mratibu wa Simba, Abbas Ally alisema yeye sio msemaji na Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ahmed Ally hakupokea wala kujibu meseji alizotumiwa na waandishi tofauti wa Mwanaspoti kutoa ufafanuzi wa suala hilo la Kibu.

Hata hivyo, hali ikiwa hivyo kwa Kibu inaelezwa kiungo mpya, Awesu Awesu na winga Willy Onana waliondoka jana kwenda kuungana na wenzao kambini wakiwa sambamba na baadhi ya viongozi wa klabu hiyo ambayo kuanzia wikiendi hii itaanza kucheza mechi za kirafiki za kujipima nguvu.

Awesu aliyesajiliwa akitoka kuwa nahodha wa KMC na Onana aliyeitwa kambini haraka ili kocha Fadlu amuangalie kisha aamue kumtema au kuendelea naye.

Mmoja ya kiongozi wa Simba amelithibitishia Mwanaspoti kuwepo kwa mechi kati ya leo ijumaa na Jumapili na baada ya hapo zitafuata mechi nyingine mbili hadi tatu kabla ya kurejea Da es Salaam.

“Baada ya mazoezi ya wiki moja kocha alianza kuonyesha mbinu zake na kuzifanyia uangalizi. Kwa zaidi ya mara mbili aliigawa timu vikosi viwili na kucheza mechi. Zilikuwa ni za ushindani na kila mmoja alikuwa na shauku ya kumuonyesha kocha ubora wake.

Pia kiongozi huyo alidokeza kampeni za uzinduzi wa tamasha la Simba Day na Jezi mpya kwa msimu wa 2024/2025 sahau kwani Mnyama anafanya mambo yake kimya kimya ili wawasapraizi wengi.

Jezi hizo zinatarajiwa kuwa na mabadiliko kadhaa ya chapa za wadhamini na wiki ijayo itakuwa ya moto kwa Simba kwani itazindua rasmi kampeni za tamasha la Simba Day ambalo kilele chake kitafanyika Agosti 03, Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Related Posts