Kulingana na afisa wa wizara ya ulinzi ya Marekani ambaye alizungumza kwa sharti la kutotajwa jina amesema mwaka 2023 kundi hilo lilihusika na mashambulizi yapatayo 121 katika katika mataifa hayo mawili.
CENTCOM hata hivyo imesisitiza kuwa kuongezeka kwa mashambulizi ya kundi hilo la kigaidi linalojiita Dola la Kiislamu huko Iraq na Syria, kunadhihirisha kuwa IS inajaribu kujiunda upya baada ya uwezo wake kupungua kwa miaka kadhaa.
Tamko la kamandi hiyo ya Marekani limetolewa ikiwa imetia tayari miaka 10 tangu kundi hilo lilipo mtangaza kwa mara ya kwanza kiongozi wao anayefahamika kama “khalifa” baada ya kuwa na udhibiti wa sehemu kubwa za Iraq na Syria.
Wakati huo, kundi hilo lilidhibiti na kutawala eneo la nusu ya ukubwa wa Uingereza ambapo lilijaribu kutekeleza kile walichokiita sheria kali ya Uislamu, na walishambulia makundi ya waumini wa dini za walio wachache na kutoa adhabu kali kwa Waislamu waliotuhumiwa kukiuka sheria za dini.
Soma pia: Wataalamu: Iraq bado ina changamoto licha ya ushindi dhidi ya kundi la IS
Wanamgambo hao wa IS waliwaua pia maelfu ya watu kutoka jamii ya walio wachache na waumi wa Yazidi na kuwateka nyara maelfu ya wanawake na watoto, wengi wao wakikabiliwa na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na biashara haramu ya binadamu.
Muungano wa zaidi ya nchi 80 ukiongozwa na Marekani, uliundwa kupambana na kundi la IS ambalo lilipoteza udhibiti wake huko Iraq mnamo mwaka 2017 na kufurushwa Syria mwaka 2019. Hata hivyo bado kunaripotiwa katika mataifa mbalimbali vikundi vidogo vyenye mafungamano na kundi hilo la kigaidi linalojiita Dola la Kiislamu.
Kwa sasa, maafisa wa Iraq wamesema kuwa vikosi vyao vina uwezo wa kukabiliana na kitisho cha IS na tayari wameanza mazungumzo na Marekani kwa lengo la kusitisha operesheni ya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani nchini Iraq. Shinikizo limekuwa likiongezeka nchini Iraq kutokana na uwepo wa vikosi vya Marekani nchini humo.
Soma pia: Operesheni ya kuwafurusha IS Anbar yaanza
Kuanzia Oktoba mwaka jana hadi hadi Februari mwaka huu, kundi la wanamgambo wenye itikadi kali ya Kiislamu wanaoungwa mkono na Iran limekuwa likiendesha mashambulizi kadhaa kwenye kambi za wanajeshi wa Marekani nchini Iraq na Syria, wakidai kuwa ni katika harakati za kulipiza kisasi kutokana na Marekani kuiunga mkono Israel katika vita vinavyoendelea katika Ukanda wa Gaza.
Mashambulizi hayo yalipungua kwa kiasi kikubwa baada ya wanajeshi watatu wa Marekani kuuawa mwezi Januari nchini Jordan katika kambi iliyo karibu na mpaka wa Syria.
Tukio hilo lilisababisha mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Marekani nchini Iraq. Siku ya Jumanne, maafisa wawili wa wanamgambo hao wa Iraq walisema kuwa wameanzisha mashambulizi mapya ya droni na kuilenga kambi ya anga ya Ain al-Asad huko Iraq. Taarifa ambayo imethibitishwa na maafisa wa usalama nchini humo na kusema kuwa droni mbili zilishambulia kambi hilo inayopatikana katika mkoa wa Anbar.