Mambo ya kuzingatia kabla ya kuanza biashara

Biashara ndogondogo zinaonekana kuwa mkombozi kwa watu wengi linapokuja suala la kupata ajira na kipato. Hata hivyo, kuanzisha na kuendeleza biashara ndogondogo si jambo jepesi. Bila kuzingatia mambo haya ni rahisi kwa biashara kufa ama kutopata mafanikio.

Asilimia kubwa ya wale ambao wapo kwenye biashara wanadhani kuwa mtaji ama kuwa na kiasi fulani cha fedha ni jambo la msingi kabisa kwenye kuanzisha biashara. Hata hivyo, kwa wengi ambao walishakuwa na biashara ndogondogo watakubaliana na mwandishi wa makala haya kuwa mtaji siyo kitu cha mwanzo kabisa cha kufikiria unapofikiria kufanya biashara. Mambo ya manne ya msingi na muhimu ni:

Moja: Kuwa na lengo la ni kwa nini unataka kuanzisha biashara na pima lengo hilo na matarajio yako kama kweli suluhisho ni kuanzisha biashara. Usianzishe biashara kwa sababu huna kitu kingine unaweza kufanya, au pengine umestaafu, au kumtafutia mtu mwingine ajira ama pengine ni kwa sababu kuna malighafi au una fedha ambazo unaweza kuzipata bure au kwa gharama ya chini. Lengo kubwa la biashara ni kupata faida, na pengine kuifanya biashara kukua.

Pili: Fikiria Kuhusiana na Soko la bidhaa au huduma unayotaka kuitoa. Ni muhimu kuangalia kwa kina na kwa muda mrefu wahitaji wa bidhaa au huduma yako unayotaka kuianzisha. Wanapendelea nini, wanaishi wapi, wana hulka zipi, na wananunua muda gani, ubora wa bidhaa au huduma, wananunua kwa kiwango gani au kipindi gani cha mwaka. Je, kuna washindani gani kwa sasa ambao wanawahudumia, soko unalofikiria na kwa wakati ujao kunaweza kuwepo na washindani gani.

Ni muhimu kujua kuwa kuna biashara ambazo zinakuwa na mvuto kipindi fulani tu cha mwaka ama mwishoni mwa mwezi au mwisho wa wiki. Hii ni muhimu na itakusaidia kupeleka bidhaa au huduma sahihi kwa watu wanaoitaka. Itakusaidia pia kuelewa biashara yako iwe sehemu gani.

Tatu: Mpango wa biashara. Huu unaweza kuwa umeandikwa ama kutokuandikwa, lakini ukiwa umefikiriwa kwa makini. Ikiwa utauweka kwenye maandishi ni vizuri zaidi. Biashara hata kama iwe ndogo namna gani kuna namna unapaswa kufikiria kuhusiana na leseni, kodi, usajili wa biashara, uendeshaji wake, namna utakaponunua bidhaa, mbinu za mauzo au mtaji wa huduma na namna utakavyoongeza thamani.

Utataka kujua unahudumia wateja wangapi kwa siku, au kwa wiki na ili kuhudumia hao wateja unahitaji vifaa gani, sehemu ipi, wafanyakazi gani wa kukusaidia kutoa huduma. Utahitaji kujua biashara inafanyika kwa utaratibu upi, mathalani kuna biashara zinahitaji kufanya manunuzi ya bidhaa mbalimbali, ama kutengeneza vifaa vinavyosaidia kutoa huduma inayotakiwa na wateja. Itakusaidia kujua gharama na kupanga bei, pia kujua mtaji wako wa biashara utakuwa kiasi gani.

Nne: Fikiria kuhusiana na namna utakavyoweza kupata mtaji na elewa vyanzo tofauti. Hakikisha unaweka hesabu ya mtaji sawa kwa kuhusisha gharama zote ili kujua unatakiwa kuwa na kiasi gani kama mtaji wa kuanzia na pia kuendeleza biashara yako. Ukihitaji mtaji huna wazo la biashara na hujafikiria kuhusiana na soko, si rahisi kuweza kupata mtaji. Mtaji unaweza kuwa ubia kwenye biashara, mkopo ama msaada wa fedha au bidhaa, sehemu ya kufanyia biashara, nk.

Ni vizuri baada ya yote hayo, kujiendeleza kwa kutafuta maarifa namna ya kulinda mtaji, kuendeleza na kuboresha biashara yako.

Related Posts