Meneja uwezeshaji biashara Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Aminiel Malisa akizungumza wakati wa kufungua mafunzo ya mawakala wa Forodha iliyofanyika jijini Dar es Salaam leo Julai 2024.
Makamu Mwenyekiti TAFFA Waheed Saudin akizungumza mara baada ya kufunguliwa mafunzo ya mawakala wa Forodha yaliyofanyika jijini Dar es Salaam leo Julai 2024.
MENEJA uwezeshaji biashara Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Aminiel Malisa amewataka mawakala wa forodha nchini kufanya kazi kwa weledi na maadili ili kuvutia uwekezaji wengi nchini na kuongeza mapato ya Serikali.
Wito huo ameutoa leo Julai 18, 2024 wakati akimuwakilisha Kamishna wa forodha katika ufunguzi wa semina kwa mawakala wa Forodha yenye lengo la kuwapitisha kwenye mabadiliko ya sheria mbalimbali kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Amesema katika utendaji wao wa kazi wanapaswa kuwa makini na kuepuka maswala yoyote ya udanganyifu na kuwa wakweli kwa wateja wao kwani wao ndio wasaidizi wa wateja hao.
“Napenda kuwakumbusha katika utendaji wetu wa kazi tunapaswa kuwa makini na kuepuka udanganyifu kwani sisi ndio wasaidizi wa wateja tunapaswa tuwe na huduma bora kwa wafanyabiashara wetu ili waweze kufurahia huduma zetu na tuweze kupata wawekezaji wengi na mapato ya serikali yaweze kuongezeka.” Amesema Malisa
Amesema kila mwaka mpya wa fedha hasa bajeti kuu ikipitishwa na bunge huja na mabadiliko mbalimbali kwenye sera ya kodi hivyo lengo kuu la semina hiyo ni kuwarahisishia wafanyabishara wanaoingiza na kutoa mizigo nje ya nchi kuwasaidia katika biashara zao na kukuza uchumi wa nchi.
Aidha amewataka mawakala hao waweze Kushirikiana na TRA ili waweze kufikia malengo kwa pande zote mbili yaani Jumuiya ya wafanyabiashara na Mawakala wa foradha.
“Tunafurahi kupitia chama chenu cha TAFFA tumekuwa tukipata ushirikiano wa karibu kwenye kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza hivyo tunaomba chama hiki kiwe kielelezo cha kuwa mfano wa kuigwa.” Amesema Malisa.
Kwa Upande wake makamu mwenyekiti wa TAFFA, Waheed Saudin amesema elimu hiyo walioipata wataenda kuwa mabalozi kwa mawakala wengine wa forodha ili kuhakikisha wanatoa huduma nzuri bora na kwa weledi ili kuongeza kasi ya ukusanyaji wa kodi ili kuchochea maendeleo kwa Taifa.