Mchepuko wamweka matatani Kyle Walker

MANCHESTER, ENGLAND: MKE wa Kyle Walker, mwanamama Annie Kilner yuko tayari kumpa ‘nafasi ya mwisho’ staa huyo wa Man City ili kuiokoa ndoa yao  lakini ni lazima beki huyo wa timu ya taifa ya England afuate masharti makali.

Mwanamama huyo ambaye kwa sasa amejitenga na mumewe, ameripotiwa kuwa yuko tayari kumpa nafasi ya mwisho Walker ili kuiokoa ndoa yao.

Kwa mujibu wa The Mirror, beki huyo wa Man City yuko katika onyo la mwisho baada ya kunaswa mara kadhaa akichepuka na mpenzi wake wa zamani, Lauryn Goodman.

Hata hivyo, nafasi hiyo ya mwisho ya Walker, 34, imekuja na masharti makali ambayo ni lazima ayafuate bila ya mjadala; likiwamo la kwamba asichepuke tena.

Hii imekuja muda mfupi baada ya Walker kufika mahakamani mapema wiki hii kwa ajili ya kesi yake na Goodman kuhusu matunzo ya watoto wao, ikiwa ni miezi kadhaa tangu kunaswa katika skendo kwamba amezaa mtoto wa pili na kimada huyo ambaye ni ‘influensa’ na pia mwanamitindo.

Licha ya kashfa hiyo, Kilner alikuwapo nchini Ujerumani kumsapoti Walker kwenye michuano ya Euro 2024, huku akionekana kuwakumbatia watoto wao wanne baada ya mechi za England.

Januari, Kilner aliweka wazi kwamba ametengana na Walker kupitia ujumbe aliouposti katika ukurasa wake wa Instagram, akisema: “Naposti hii kutokana na kuongezeka kwa maswali ya vyombo vya habari kuhusu ndoa yangu na Kyle na katika juhudi ya kuilinda familia yangu dhidi ya presha ya vyombo vya habari. Ni mbaya kwamba baada ya miaka mingi na kupata watoto wengi pamoja; nimeamua kuchukua muda wangu kukaa mbali na Kyle.”

Hata hivyo, huenda sasa wameyajenga.

Wakati vita ya mahakamani ya Walker na Goodman ikitarajiwa kuendelea, beki huyo wa England atakwenda mapumzikoni baada ya kazi kubwa ya kuifikisha timu hiyo hadi fainali ya michuano ya Euro, ambako walifungwa 2-1 na mabingwa Hispania. Kisha Walker atarejea kwenye kambi ya klabu yake ya Man City ndani ya wiki chache zijazo.

Related Posts