Mnigeria atua Fountain Gate | Mwanaspoti

Fountain Gate imekamilisha uhamisho wa aliyekuwa kipa wa Tabora United raia wa Nigeria, John Noble kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Kipa huyo aliyejiunga na kikosi hicho Julai 31, mwaka jana akitokea Klabu ya Enyimba ya kwao Nigeria, amemaliza mkataba wake na Tabora United huku kukiwa hakuna mazungumzo mapya na kuifanya Fountain Gate kutumia fursa ya kuinasa saini yake.

“Tumekamilisha uhamisho wake na muda wowote kuanzia sasa atajiunga na wenzake katika kambi yetu ya maandalizi ya msimu mpya hapa Babati mkoani Manyara, tumepata kipa mzuri na mzoefu atakayetusaidia,” alisema mmoja wa viongozi wa Fountain.

Akizungumza na Mwanaspoti, Noble alisema kwa sasa ni mapema sana kuzungumzia timu atakayoichezea msimu ujao ingawa muda utakapofika mashabiki zake watafahamu, huku akiweka wazi zipo timu nyingi hadi sasa zilizojitokeza kuhitahi saini yake.

Kwa upande wa Rais wa Fountain Gate, Japhet Makau alisema, watahakikisha wanaendelea kuboresha timu kwa kuingiza majina makubwa na yenye tija, wanayoamini yatakuwa na msaada mkubwa kwa msimu ujao wa mashindano mbalimbali hasa Ligi Kuu Bara.

Noble anakuwa ni uhamisho wa pili wa timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao, baada ya awali kupata saini ya aliyekuwa nyota mshambuliaji na mfungaji bora wa Ligi ya Zanzibar (ZPL) msimu uliopita, Seleman Mwalimu Gomez aliyetokea Klabu ya KVZ.

Msimu uliopita Gomez akiwa na kikosi cha KVZ alionyesha uwezo mkubwa na aliibuka mfungaji bora wa Ligi ya Zanzibar (ZPL), baada ya kufunga jumla ya mabao 20 na kuchangia mengine saba ‘Assisti’ katika michezo 27, kati ya 30, aliyocheza.

Related Posts